Searching...
Image and video hosting by TinyPic
27 December 2014
Saturday, December 27, 2014

Wazee wa Mtani Jembe hoi kwa Kagera Sugar



Na Oscar Oscar Jr

Kagera Sugar wameendelea kuwa wababe wa vigogo wa ligi kuu Tanzania bara baada ya msimu huu kuziangushia vipigo timu za Simba na Yanga huku wakitoka sare na vinara wa ligi hiyo timu ya Mtibwa Sugar.

Baada ya kushuka dimbani mara saba bila kupoteza mchezo wowote, Atupele Green alikuwa mwiba mchungu kwa vijana hao wa mtaa wa Msimbazi baada ya kufunga bao moja na la pekee kwenye mchezo huo ambao haukuwa wa kuvutia sana kutokana na mpira muda mwingi kuwa nje ya uwanja.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Andrew Shamba wa Pwani, hadi mapumziko Kagera Sugar walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga B, Atupele Green.

Atupele alifunga bao hilo kwa shuti akimalizia mpira wa kurushwa na Benjamin Asukile, ambao kabla ya kuingia nyavuni ulimbabatiza beki wa Simba SC, Hassan Isihaka.  


Bado kipa wa Simba, Ivo Mapunda aliendelea na makosa yake madogo madogo ambayo yamekuwa mara kadhaa yakiigharimu Simba.

Matokeo hayo yanawafanya Simba kubakia na pointi tisa huku Kagera Sugar ambao jana ulikuwa ni mchezo wao wa tatu kushinda msimu huu, wametimiza alama 13 ambazo ni sawa na Yanga wanaoshika nafasi ya pili na Azam waliopo kwenye nafasi ya tatu.

Simba wanajipanga kwa mchezo unaofuata ambapo watakuwa ugenini kwenye dimba la Mkwakwani-Tanga kucheza na Mgambo JKT huku Kagera Sugar wao, wataendelea kucheza ugenini na sasa watashuka Mkoa wa Pwani kuwakabili Ruvu Shooting.


0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!