Searching...
Image and video hosting by TinyPic
18 October 2014
Saturday, October 18, 2014

Maximo anawachezaji lakini hana timu.



 Na Samuel Samuel

Kocha wa Simba Patrick Phiri ameiingiza timu uwanjani akifikiria kujilinda zaidi kuliko kuiacha timu ifunguke. Kufanikisha hilo alicheza vizuri na saikolojia ya Peter Manyika ambaye ni kipa chaguo la tatu. 

Alionesha kumwamini na kumtengenezea ulinzi mzuri kwa kumpangia wachezaji ambao kwa kiasi kikubwa wameinyima Yanga ushindi kutokana na kujiamini kwao.

Ingawa Phiri aliingia uwanjani kujilinda zaidi lakini aliamini njia nzuri ya kujilinda ni kushambulia. Hivyo alitumia mfumo mama wa soka ambao upo 50/50 kiulinzi na kushambulia. 

Wakati Maximo akitumia 4-1-3-2-1 , Phiri aliacha timu icheze kwa 4-4-2 huku Kiungo mkabaji Jonasi Mkude akisaidiwa vizuri na Isiaka sehemu ya kati na  Mohamed Hussein upande wa kushoto. 

Mabeki hawa wa mwisho na kiungo mkabaji wa Simba Mkude, waliikata Yanga vizuri kulikaribia lango lao. Kuonesha Phiri aliisoma vizuri saikolojia ya Maximo, dk ya 34 alimtoa nje Said Ndemla ambaye alikuwa akicheza winga ya kulia lakini alishindwa kutengeneza pasi nzuri za mwisho kwa Kiemba . 

Phiri alimwingiza Kisiga ambaye ameonesha uwezo mzuri wa kutengeneza nafasi na kumsaidia Kwizera pale kati baada ya Mkude kutoka. 

Labda tuseme Phiri alichelewa kumwingiza Singano ambaye dakika 10 alizopata baada ya kutolewa Kiemba,alionesha uwezo mzuri wa kuichachafya ngome ya Yanga. 

Maximo ajilaumu mwenyewe kwa kukubali kujipeleka mwenyewe kwenye ngome ya Phiri. Mfumo aliotumia Maximo umeigharimu Yanga kupata ushindi na kujikuta mtumwa wa kucheza counter na kuzuia mashambulizi ya Simba. 

 Maximo ametumia 4-1-3-2 . Mfumo huo uliifanya Simba kutawala kiungo chote. Mbuyu Twite amepata kazi kubwa kupandisha timu maana alicheza chini kuliko kusogea mbele ambapo Mkude, Ndemla na Okwi waliziba njia na kupata msaada mzuri wa Isiaka na Mohamedi Hussein. 

Mfumo wa Maximo umemnyima uhuru wa kucheza Niyonzima. Amejikuta akirudi nyuma sana kumsaidia Twite na hali hiyo iliifanya fowadi ya Yanga kukosa muunganiko mzuri toka nyuma na kujikuta wakihaha kutafuta mipira. 

Andrey Coutinho hakupaswa kucheza dakika zote 90, ameonesha bado ana uoga wa kupenya kwenye ngome ya mabeki, na kitendo cha kukaa na mpira muda mrefu kuliziba move za goli. Naweza sema Maximo ana wachezaji wa ushindi lakini hana timu ya ushindi. 

Yanga inakosa plan za kutengeneza magoli. Jaja kama mshambuliaji wa kati kushindwa kuwa na kasi na ubunifu pale anapobanwa , anapunguza kasi ya Yanga kufunga .

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!