Searching...
Image and video hosting by TinyPic
27 December 2014
Saturday, December 27, 2014

Simba mlinidanganya kwa Mtani Jembe



Na Peter Richard Kabita

Kama una roho nyepesi na una matatizo ya moyo, ni heri usiwe mfuasi wa soka hasa kwa soka la bongo. Soka letu limejaa mizengwe, limejaa fitina na hakuna hata dalili moja inayoashiria kama tumeanza kuelekea njia kuu!

Watu wanakwambia mpira ni mchezo wa makosa, huu ni uongo mkubwa. Mpira ni sayansi tena kali yenye mbinu na ufundi wa hali ya juu.Timu zetu zinaonekana kufanya vizuri leo, kesho kiwango kinashuka. Unajua tatizo? Sayansi bado haijatuingia.

Ushawahi kujiuliza kwanini timu za wenzetu zinaajiri kabineti za ufundi kwa gharama kubwa? mpira ni mipango, mpira ni ufundi,  mpira ni mbinu.  

Kama ungekuwa mpira ni mchezo wa makosa watu wasinge ajiri mkocha kwa gharama kubwa. Wangecheza tu wenyewe wasubiri flani akosee wao wafunge.

Kuna siku moja nikiwa mkoani Geita nikitafuta usafiri wa kuelekea katika kijiji cha Nzera ambacho kina patikana kama umbali wa kilomita 45.

Nilitafuta gari ambalo lilikuwa na muonekano mzuri huku nikiamini kuwa safari yangu itakuwa nzuri na salama. Basi linang'aa kwa rangi za ndani na siti ni mpya kabisa!

Huwezi kuamini, kilometa 45 tulitumia masaa matatu sio kwamba barabara mbovu ila gari lilikuwa kimeo. Kila baada ya dakika tano gari lilichemsha na yale yote niliyoyaacha stend kwa kuyaona mabovu yalitupita njiani.

kila nikikumbuka ile safari, naikumbuka mechi ya simba dhidi ya Kagera Sugar iliyopigwa jana uwanja wa Taifa na Kagera Sugar wakafanikiwa kuondoka na alama tatu baada ya kupata ushindi wa goli 1-0.

Inashangaza kwa kweli Simba hii iliyosheheni wachezaji tunaowaita "Mapro" kuona wakiruka ruka tu uwanjani! Unageweza kumtafuta jana alipo Danny Sserunkuma na usimuone. Ungeweza kumtafuta alipo Okwi na usipate jibu! Simba walikuwa chini ya kiwango.

Simba niliyoiona kwenye mechi ya mtani jembe dhidi ya Yanga, ilikuwa ni Basi jipya. Kila mtu angeshawishika kupanda. Kila mtu alikuwa na matumaini makubwa lakini kwa nilichokiona jana, sioni tofauti yao na Basi nililopanda kwenda kijiji cha Nzera nikitokea Geita.

Kumbe Simba walinidanganya na rangi za kupendeza, kumbe Simba walinidanganya na siti zao za kuvutia. Simba ya jana haikuonyesha tumaini jipya, imewatia hofu wapenzi na wanachama wake.

Pamoja na hayo yote, bado kocha ana muda wa kurekebisha  mapungufu yaliyojitokeza na hatimaye wakaimarika kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Mgambo Shooting utakaochezwa ugenini ndani ya jiji la Tanga.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!