Wasiwasi watanda kwenye kikosi cha Man City.
Na Oscar Oscar Jr
Kocha Manuel Pellegrini ameendelea kuchanganyikiwa baada ya kuibuka taarifa kuwa, kuna uwezekana akawakosa David Silva na Yaya Toure kuelekea mpambano wa watani wa jadi kati yao na majirani zao, timu ya Manchester United.
Wasiwasi huo umeibuka baada ya David Silva kupata majeruhi kwenye mchezo wao dhidi ya Newcastle United ambao ulimalizika kwa Mabingwa watetezi wa taji hilo, Manchester City kufungwa bao 2-0.
Silva aliumia mapema mnamo dakika ya nne ya mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Samir Nasri ambaye alikuwa nje kwa majeruhi tangu mwezi Septemba.
Wanahabari walionekana kumlaumu kocha huyo kwa kumchagua David Silva kwenye mchezo huo, wakati anajua fika siku ya jumapili kutakuwa na mechi ngumu dhidi ya mahasimu.
Kufuatia tuhuma hizo Pellegrini amejitetea na kusema, hakukuwa na tatizo lolote kwani kulikuwa na siku nne za kupumzika kabla ya Derby hiyo hivyo, Silva angeweza kupata tu muda wa kutosha wa kupumzika.
Manchester City watalazimika kusubiri hadi siku ya Alhamisi ili kujua kama Silva na Yaya watakuwa fiti kwa ajili ya mechi hiyo.
Manchester City wako kwenye nafasi ya tatu wakiwa na alama 17 baada ya kupoteza mechi yao dhidi West Ham United mwishoni mwa wiki iliyopita huku, Manchester United wakiwa kwenye nafasi ya nane baada ya kutoka sare na Chelsea ya 1-1 kwenye dimba la Old Trafford.
0 comments:
Post a Comment