Searching...
Image and video hosting by TinyPic
28 November 2014
Friday, November 28, 2014

UKOLONI MAMBO LEO KWENYE SOKA LETU



Na Samuel Samuel
 0652464525

Muheshimiwa Joel Bendera akiwa bado kijana kabisa mwaka 1980 aliiandikia historia ya kipekee nchi hii baada ya kuiwezesha kufuzu kucheza mashindano ya mataifa huru ya Afrika. Ni zaidi ya miaka 30 hakuna kocha mwingine aidha mzawa au kutoka nje aliye jaribu kuifikia historia hiyo. 

Muheshimiwa huyo kwa sasa ni mkuu wa mkoa wa Morogoro baada ya kuachana na soka na kujikita kwenye siasa. Siasa za dunia hasa katika suala la utandawazi kwa kiasi fulani nchi za Afrika, tunaburuzwa tu. 

Tunashindwa kuelewa tafsiri sahihi ya kuendana na mifumo hiyo ambayo kwa namna moja ama nyingine, imejengwa kwa sisi kuthamini vya kwao na mambo yetu kuyaona hayana utashi na ubora kama wao. 

 Dhana hiyo ndo kwa kipindi kirefu tumekuwa tukithamini makocha toka nje kuliko wakwetu. Makocha wetu wamebaki kuwa makocha wasaidizi kwenye vilabu vyetu vikubwa na timu yetu ya Taifa. 

Kama Bendera miaka ya 80 akiwa na damu halisi ya kitanzania aliweza kuipeleka nchi yetu Afcon na tumekaa zaidi ya miaka 30 bila hata kusikia harufu ya mashindano hayo achilia mbali kombe la dunia, kwanini tusiwaamini tena makocha wetu?

Tunashindwa kuwaamini kwa sababu tumefunikwa na kilemba cha ukoloni mambo Leo. Kocha mpaka atoke nchini Brazil, Serbia , Zambia na kwingineko ndiyo anaaminika kufundisha. Tunawavunja sana moyo makocha wetu. 

Ni nani asiyetaka kufikia kilele cha mafanikio yake? Wakati makocha wengine kwenye nchi zao wanajitahidi kusoma zaidi na kuvipa mafanikio vilabu vyao ili mwisho wa siku waitwe kuzinoa timu zao za Taifa.

Tanzania ni ndoto hata kufundisha Azam FC , Simba na Yanga. Kweli Leo Yanga inashindwa kumwamini Charles Mkwasa kuinoa klabu hiyo? 

Kama Bendera katika ujana wake aliipeleka Stars Afcon, Je ni lini Mexime ataaminiwa na kukabidhiwa stars? Kila msimu amekuwa imara kudhalisha vipaji vipya na msimu huu yupo kileleni na Mtibwa yake akiwa na pointi zake 15 mbele ya Azam, Simba na Yanga zote zenye makocha toka nje, wako nyuma yake. 

Tuwathamini wazawa wetu kwa kuwajengea dhana ya ushindani na kuwalipa vizuri. Kila mmoja atafanya bidii ili siku moja aifundishe Yanga, Simba , Azam na baadaye Stars.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!