Meneja wa Arsenal Arsene Wenger ni kama amekiri kwamba hawawezi
kushinda ligi na ameonya kuwa sasa wanalazimika kuangazia kumaliza
katika nne bora baada ya kulazimishiwa sare ya 2-2 nyumbani na Swansea
City kwenye Ligi ya Premia Jumanne.
Vijana hao wa Wenger walianza wiki moja iliyopita wakiwa miongoni mwa
wanaopigania taji lakini wameteleza baada ya kutwangwa 6-0 na viongozi
Chelsea mechi ya 1 000 Wenger akiwa meneja wa timu hiyo Jumamosi na sare dhidi ya
Swansea iliyotokana na bao la kujifunga dakika za mwisho lake Mathieu
Flamini.
Arsenal sasa wako alama sita mbele ya Everton walio wa tano, ambao
walilaza Newcastle 3-0 Jumanne na wana mechi ambayo hawajacheza, huku
wakipigania nafasi ya kushiriki Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.
"Kushinda taji si hofu kubwa kwetu sasa,” Wenger aliambia kikao cha wanahabari.
“Lazima tuongee ukweli. Lazima sasa tutazame nyuma yetu. Everton
walishinda, na bila shaka, sasa lazima tungazie mechi yetu ijayo
(nyumbani dhidi ya Manchester City).
"Manchester City walipata matokeo mazuri leo usiku (ushindi wa 3-0
Manchester United). Wanaonekana kuwa moto. Wao na Chelsea ndio
wanaopigiwa upatu sasa kushinda taji. Hatuna nafasi sasa ya kurudi
mbioni.
Chelsea wana alama 69 kutoka kwa mechi 31 mbele ya City walio na
alama 66 kutoka kwa mechi 29, huku Liverpool wakiwa nambari tatu na
alama 65 kutoka mechi 30, Arsenal wa nne na alama 63 kutoka mechi 31 nao
Everton alama 57 kutoka kwa mechi 30.
Nafasi ya Arsenal eneo la kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya
inaonekana kuwa hatarini zaidi ikizingatiwa kwamba Manchester City
watatua The Emirates Jumamosi kabla ya vijana hao wa Wenger kwenda
Everton Aprili 6.
"Matokeo hayo yanavunja moyo,” alisema Wenger. “Tukiwa 2-1 labda
tuliogopa sana kwa sababu kujiamini kwetu kuliathiriwa na matokeo ya
Jumamosi na tulitaka kushinda tu mechi bila kujitokeza sana na
kushambulia.”
"Kosa lilitendeka na likapelekea matokeo ambayo hatukuyataka usiku huu.”
26 March 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment