Na Chikoti Cico
Mshambuliaji wa klabu ya Chelsea Diego Costa amekutwa na hatia na chama cha soka nchini Uingereza (FA) baada ya kushtakiwa kwa kosa la kumkanyaga Emre Can kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili ya kombe la Capital One uliochezwa mapema wiki hii kwenye uwanja wa Stamford Bridge.
Costa alishtakiwa na FA Jumatano ya wiki hii baada ya mchezo huo dhidi ya Liverpool lakini alikataa shtaka hilo huku klabu ya Chelsea ikisema tukio hilo lilikuwa ni bahati mbaya.
Taarifa ya FA kuhusu adhabu hiyo inasema “Diego Costa atatumikia michezo mitatu ya kusimamishwa mapema baada tu ya mashtaka ya kitendo cha vurugu dhidi yake kupatikana na hatia na kamati huru ya marekebisho (independent regulatory commission) leo, (Januari 30, 2015)”.
“Mshambuliaji wa Chelsea alikataa shtaka kuhusiana na tukio la nje ya uwanja llinalomhusisha Emre Can wa Liverpool ambalo lilotokea kwenye dakika ya 12 ya nusu fainali ya pili ya kombe la ligi kwenye uwanja wa Stamford Bridge Jumanne Januari 27, 2015. Tukio halikuonwa na waamuzi wa mchezo lakini lilidakwa kwenye video”.
Mshambuliaji huyo ambaye ameifungia Chelsea magoli 17 mpaka sasa kwenye ligi kuu nchini Uingereza ataanza kutumikia adhabu hiyo kwenye mchezo dhidi ya Manchester City Jumamosi ya kesho kwenye uwanja wa Stamford Bridge na michezo ya tarehe 7 Februari dhidi ya Aston Villa ugenini na Februari 11 dhidi ya Everton nyumbani.
0 comments:
Post a Comment