KAMA ILITOKEA KWA GUTIERREZ HAITASHINDIKANA KWA MKUDE.
Na Chikoti Cico
Mapema mwezi wa tisa mwaka huu, dunia ilipokea taarifa za kusikitisha toka nchini Argentina zikimhusisha kiungo wa Newcastle United, Jonas Gutierrez kuhusu ugonjwa aliokuwa nao wa kansa ya makende.
Habari hii ilikuja baada ya kupata maumivu yasiyokoma kwenye korodani toka mwezi wa tano mwaka 2013 kabla ya kufanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa na uvimbe kwenye korodani.
Huku ikiwa ni kwenye hatua za mwanzoni kabisa za ugonjwa huo, Gutierrez alirejea nyumbani kwako Argentina ili kuweza kutibiwa na baada ya miezi miwili mchezaji huyo kipenzi cha mashabiki wa Newcastle, ameweza kupona na taratibu anatarajiwa kurejea kufanya mazoezi na timu hiyo kwa siku za usoni.
Huyu ni mchezaji wa kulipwa ambaye kila mara huwa anafanyiwa vipimo vya afya lakini ugonjwa aliokuwa nao uligundulika baada ya kugongana na beki wa Arsenal, Bacary Sagna na kuumia viungo vya uzazi wakati Newcastle walipokutana na Arsenal kwenye moja ya mechi za ligi kuu nchini Uingereza.
Inashangaza lakini ukweli ndiyo huo kwamba kilichofanya ugonjwa huo ugundulike ni maumivu Gutierrez aliyokuwa akiyapata baada ya kugongana na Sagna na baada ya maumivu hayo makali kumsumbua kwa muda mrefu.
Huku hayo yakitokea katika nchi zinazojulikana kuwa na vifaa bora vya upimaji wa magonjwa na mazingira stahiki ya kujali afya za wachezaji, sasa narejesha fikra zangu nchini Tanzania na nawaza aina ya hospitali tulizonazo na vifaa vya upimaji tulivyonavyo halafu nawaza afya za wachezaji wetu, nabaki kutikisa kichwa tu.
Ndiyo nabaki kutikisa kichwa tu kwa huzuni. Kwasababu kila kabla ya msimu mpya wa ligi usajili wa wachezaji unafanyika na kati kati ya msimu pia lakini hutasikia mchezaji akifanyiwa vipimo vya afya na wala hakuna anayetaka kujua hilo na pia wakati ligi ikiendelea hakuna upimaji wowote unaondelea kujua ufiti wa wachezaji. (Angalau Azam fc, wamezinduka kwa sasa)
Hivi karibuni, mchezaji Jonas mkude amesaini mkataba wa miaka miwili na timu ya Simba kwa dau la Shilingi milioni 60 na anatarajiwa kupewa mshahara wa kiasi cha shilingi milioni 2 kila mwezi na kwa mara ya kwanza mkataba wake umehusisha kukatiwa bima ya afya.
Bado unawaza mbona hakuna taarifa zozote za kufanyiwa uchunguzi wa afya kabla ya kusaini mkataba mpya ama ndiyo bora punda afe mzigo ufike?.
Tunaweza kubishana sana katika hili lakini ukweli utabaki pale pale kwamba, uendeshaji wa soka la kisasa unatakiwa kwenda sambamba na wachezaji kujali afya zao lakini pia timu kuchukua jukumu la kuwapima afya wachezaji ambao wanataka kuwasajili kwa manufaa yao na manufaa ya mchezaji mwenyewe.
Lakini pia ni vyema wachezaji kujua umuhimu wa kuwa na bima ya afya kama sehemu ya huduma anazotakiwa kupata anaposajiliwa na sio kuweka kipaumbele kupata Prado ama Toyota Mark II huku afya ikiwa inazorota.
Leo Gutierrez anarejea uwanjani baada ya kuwa kwenye vita kali ya kupigania afya yake nje ya uwanja, wapenzi wa soka tunapenda kuona wachezaji wakiwa uwanjani wakitupa burudani na tusingependa kuona Msuva, Mkude, Kiprecheche ama mchezaji yeyote yule kwenye ligi kuu akiwa nje ya uwanja kwasababu ya kusumbuliwa na maradhi ambayo yangeweza kuepukika mapema.
0 comments:
Post a Comment