KIPA mahiri ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao hauna timu kwenye Ligi Kuu Bara, Deo Munishi ‘ Dida’, amejifunga Yanga baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili ingawa ule wa awali utamalizika mwishoni mwa msimu.
Hata hivyo, Mwanaspoti linajua kwamba wachezaji wa kigeni, Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima wanaendelea na mazungumzo na viongozi wa Yanga juu ya kusaini mikataba mipya na imeelezwa kuwa mazungumzo hayo yamefikia pazuri.
Kigogo mmoja mwenye ushawishi mkubwa na anayehusika na utendaji wa Yanga, aliliambia Mwanaspoti kuwa, Niyonzima ataongeza mkataba wa miaka miwili, lakini kwa upande wa Twite bado wanafanyia marekebisho mengi kwenye mkataba wake mpya, ingawa hana wasiwasi wa kusaini mkataba mpya kwa vile kocha ana malengo naye ya muda mrefu.
Alisema wameamua kuanza mazungumzo mapema kutokana na umuhimu wa wachezaji hao katika timu ili wasije wakawapa nafasi wapinzani wao kuwasajili kwani muda uliobakia wanaruhusiwa kuzungumza na klabu nyingine.
Source: Gazeti la Mwanaspoti.
0 comments:
Post a Comment