Na Oscar Oscar Jr
Ligi kuu ya Uingereza inatarajiwa kutimua vumbi lake tena kuanzia Jumamosi wiki hii kwenye viwanja mbali mbali baaada ya kusimama kwa muda ili kupisha michuano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ile ya kufuzu michuano ya Euro na Mataifa ya Afrika.
Chelsea ambao ndiyo vinara wa ligi hiyo, watashuka dimbani siku ya Jumamosi kuwakaribisha West Bromwich Albion kwenye dimba la Stanford Bridge saa 12 Jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Chelsea ambao hawajapoteza mchezo hata mmoja msimu huu, watakutana na timu ya West Brom ambao wanashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Kwa upande wa bingwa mtetezi, Manchester City wao watakuwa nyumbani kwenye dimba la Etihad kuwaalika Swansea City ambao, mchezo uliopita wametoka kuwafunga Arsenal kwa bao 2-1.
Manchester City ambao wameshapoteza michezo miwili ya ligi kuu, watahitaji kushinda mchezo huo ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao.
Pale Goodison Park, Everton ambao wanashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi kuu baada ya kushinda mechi tatu kati ya 11 zilizopigwa mpaka sasa, watawaalika West Ham United ambao wameonekana kuwa kwenye ubora wa juu huku wakishika nafasi ya nne kwenye ligi baada ya kujikusanyia alama 18 mpaka sasa.
Leicester City ambao walianza ligi kwa kasi, wanaonekana kuanza kupoteana huku wakipoteza michezo sita na kushinda mmoja tu, watalazimika kushinda mchezo wao dhidi ya Sunderland ili kujinasua kwenye mstari wa timu zinazoweza kushuka daraja. Leicester City wako nafasi ya 18 huku, Sunderlanda wakishika nafasi 14.
Newcastle United ambao wanaonekana sasa kuzinduka baada ya kuwa na mwanzo mbaya wa ligi, watakuwa nyumbani kwenye dimba la St.Jame's Park kuwakaribisha watoto wa babu, Harry Redknapp timu ya QPR ambao wameshafungwa mechi nyingi kuliko timu zote (7).
Newcastle baada ya kushinda mechi zao za hivi karibuni, wamepanda na kwa sasa, wanashika nafasi ya nane.
Katika dimba la Britania, kutakuwa na mchezo kati ya wenyeji Stoke City ambao watawakaribisha timu ya Burnely, mchezo utakaoanza majira ya saa 12 Jioni kwa saa za kwetu.
Stoke wanashika nafasi nafasi ya tisa kwenye ligi huku wakiwa wameshinda mechi nne kati ya 11 walizocheza.
Burnley wanakamata mkia kwa kuwa nafasi ya 20 huku wakionyesha udhaifu mkubwa kwenye safu yao ya ulinzi ambapo mpaka sasa, wameruhusu kufungwa magoli 19.
Hali si shwari na kama kweli wanataka kubakia ligi kuu ni lazima washinde mchezo huo na kuwafanya wafikishe pointi 10 ambapo kwa sasa wana saba pekee.
Siku hiyo ya Jumamosi, itahitimishwa kwa mchezo kati ya Arsenal dhdi ya Manchester United, mchezo utakaofanyika majira ya saa 2:30 Usiku ndani ya dimba la Emirates.
Arsenal kwa misimu ya hivi karibuni, wamekuwa hawapati matokeo ya ushindi wanapocheza na Man United lakini, Majeruhi yanayowakabili United, yanaweza kubadilisha historia kuelekea mchezo huo.
Arsenal kwa sasa wanashika nafasi ya sita kweye msimamo wa ligi kuu huku, Manchester United ambao bado hawajakuwa sawa wanashika nafasi ya saba.
Kama Man United ataibuka na ushindi, atakuwa anajiweka kwenye mazingira mazuri kuelekea kusaka moja ya nafasi nne za juu huku ushindi kwa Gunners, utawarejesha tena kwenye mbio za kusaka ubingwa ambapo Chelsea na Southampton wanaonekana kama timu ambazo hazikamatiki.
0 comments:
Post a Comment