Chelsea wakichafua mbele ya Stoke City.
Na Oscar Oscar Jr
Hatimaye Xmass imekuwa njema kwa vinara wa ligi kuu Uingereza, timu ya Chelsea baada ya kupata ushindi wao wa 13 msimu huu na kufikisha pointi 42 ligi kuu ya Uingereza.
Ushindi huo dhidi ya Stoke City wa mabao 2-0 ulianzishwa na nahodha wa timu hiyo, John Terry ambaye alifunga bao la kwanza mnamo dakika ya pili tu ya mchezo na baadaye, Cesc Fabregas akafunga la pili na kuwafanya Stoke City kupoteza mchezo wao wa nane msimu huu.
Manchester City wanaendelea kushika nafasi ya pili baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wao wa siku ya Jumamosi dhidi ya Crystal Palace wa mabao 3-0 matokeo yaliyofanya watimize alama 39.
Baada ya Manchester United kutoka sare dhidi ya Astoni Villa siku ya Jumamosi, walifikisha alama 32 zilizowaweka kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo ambayo inaelekea kumaliza mzunguko wa kwanza.
Mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Britania, ulishuhudia wachezaji watatu wa Stoke City wakilambwa kadi za njano huku umiliki wa mpira asilimia 51 zikienda kwa Stoke City na Chelsea kuambulia 49 pekee kwa mujibu wa bbbc sports.
Mchezo huo pia ulishuhudia matumizi ya nguvu kwa wachezaji wa Stoke City na kupelekea kucheza madhambi mara 11 huku Chelsea wakifanya hivyo mara nne pekee.
Mpaka sasa Chelsea ndiyo timu inayoongoza kwa kuwa na safu bora ya ushambuliaji kwani tayari wameshafunga magoli 38 ambayo hayajafikiwa na timu yoyote huku wao na Southampton pia ndiyo timu pekee zilizoruhusu mabao machache ya kufungwa (13).
0 comments:
Post a Comment