Searching...
Image and video hosting by TinyPic
16 November 2014
Sunday, November 16, 2014

AVEVA NA MANJI JIFUNZENI KWA MIKE ASHLEY.



Na Chikoti Cico


Mwandishi wa Mashahiri na Mwanaharakati kutoka Marekani, Maya Angelou aliwahi kusema “Tough times never last but tough people do” akimaanisha “Nyakati ngumu hazidumu lakini watu wagumu hudumu” 

Inawezekana haya ndiyo maneno yaliyompa nguvu kocha wa Newcastle United, Alan Pardew alipokumbwa na kipindi kigumu cha matokeo mabovu ya timu yake kwenye ligi kuu ya nchini Uingereza.

Mpaka mwanzoni mwa mwezi wa kumi, timu ya Newcastle ilikuwa haijashinda mchezo wowote wa ligi huku ikiwa imejikusanyia alama nne tu katika michezo saba.

Ni matokeo mabovu ambayo yaliamsha hasira za mashabiki  wa timu hiyo maarufu kama “toon” mpaka kufikia hatua ya kuanzisha mtandao ulioitwa “sackpardew.com” yani “mfukuzepardew.com”.

Lakini wakati mashabiki wakishinikiza kocha huyo afukuzwe kazi mmiliki wa timu ya Newcastle, Mike Ashley wala hakuwa na habari nao.

Akiwa na shati lake jeupe kwenye eneo la VIP akiangalia mechi za timu yake pamoja na matokeo mabovu, bado alikuwa upande wa Kocha Pardew na wala hakutaka kuwasikiliza mashabiki.

Kwa kuaminiwa huko na mmiliki wa timu, kulifanya presha ya kocha Alan Pardew ipungue na akaweza kuifanya kazi yake akiwa na utulivu na hatimaye, timu ya Newcastle ikaanza kupata matokeo mazuri kwani mpaka sasa Newcastle inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 16 huku ikishinda michezo mitano mfululizo na moja ya michezo hiyo ni kwa kuifunga na kuitoa timu ya Manchester City kwenye mashindano ya kombe la Capital One. 

Hali ambayo Newcastle imekutana nayo toka mwanzoni mwa ligi ya Uingereza unaweza kuifananisha na hali ya timu zetu za hapa Tanzania kwenye ligi kuu ya Vodacom.

Ukiangalia toka ligi imeanza timu zetu za kariakoo Simba na Yanga zimekuwa na mwanzo mgumu wa ligi huku Simba ikipata sare tano mfululizo na Yanga kupoteza michezo miwili hali ambayo si ya kawaida kwa timu hizi.

Lakini tayari makocha wa timu hizo walikuwa kwenye shinikizo la kufukuzwa kazi huku Simba wakifika mbali kabisa na kumpa kocha Phiri idadi ya mechi ambazo asiposhinda atafukuzwa!

Hiyo inaonyesha ni jinsi gani ambavyo tunakosa uvumilivu na makocha tulionao katika kipindi kifupi cha ligi na hii husababishwa na matamanio ya viongozi kupata matokeo mazuri ya haraka haraka ili kuweza kujisifu kwenye mikutano ya vilabu vyao bila kujali mipango ya kocha.

Sina ajenda ya siri ya kuwatetea makocha wabovu ila katika mpira wa dunia ya leo ni ngumu kocha kuhukumiwa kwa kuangalia mechi tano tu za ligi wakati mfano ligi ya VODACOM kuna jumla ya mechi 26.

Ni muhimu kwa viongozi wa soka letu hasa wa vilabu vya Simba na Yanga kuwapa makocha wao muda wa kufanya kazi huku wakiwaunga mkono lakini zaidi sana kuacha mipango yote inayohusu upangaji wa vikosi, usajili wa wachezaji kubaki chini ya mamlaka ya makocha pekee.

Mike Ashley ametoa somo zito kwa viongozi wa soka letu hapa bongo hasa kwa Evance Aveva na Yusuph Manji ambao ni viongozi wa vilabu vikubwa nchini, Ashley ameonyesha umuhimu wa viongozi kumuunga mkono kocha hasa wakati timu inapitia nyakati ngumu.

NAWASILISHA

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!