Searching...
Image and video hosting by TinyPic
3 January 2015
Saturday, January 03, 2015

Hao ndiyo wanaowindwa na Liverpool kwa sasa.


 Na Oscar Oscar Jr

Liverpool ambao wanakamata nafasi ya nane kwenye ligi kuu nchini Uingereza huku wakiwa wameshafunga mabao 28 mpaka sasa kwenye mechi 20, wamejipanga kuhakikisha wanaongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ambayo imeonekana kusua sua baada ya kuumia kwa Danniel Sturridge na kushindwa kung'aa kwa Mario Balotelli.

Liverpool wametajwa kuwa kwenye rada za kumnasa mshambuliaji wa zamani wa Tottenham Hotspurs, Jemain Defoe ambaye kwa sasa anakipiga na klabu ya Toronto ya huko nchini Marekani. 

Defoe 32 anaonekana kuwa tayari kurejea kwenye ligi kuu ya Uingereza lakini tatizo linaloweza kukwamisha mpango huo ni kwamba, Toronto wanataka kumuuza moja kwa moja huku Liverpool wakimuhitaji kwa mkopo tu.

Mbali na Liverpool, timu za Hull City na QPR nazo zinamtaka na hasa QPR ambapo kocha Harry Redknapp, anataka kuungana na mchezaji wake huyo wa zamani licha ya kuwa na Charlie Austin ambaye mpaka sasa ameshaifungia QPR mabao 12 ya ligi kuu.

Tatizo la Defoe kutua QPR linatajwa kuwa mshahara wake wa Pauni 60,000 kwa wiki kitu ambacho kwa bajeti ndogo aliyopewa Redknapp inaonekana kuwa vigumu kumnasa mshambuliaji huyo.

Kwa upande wa pili, Liverpool wamejitosa kumuwania mshambuliaji wa Swansea City, Wilfredy Bonny ambaye mpaka sasa ameshafunga mabao tisa lakini bei anayouzwa ni Pauni 30M. 

Huyu ni mshambiliaji amabaye klabu nyingi zinamtolea macho kwa sasa huku kukiwa pia na taarifa za kutakiwa na klabu za Real Madrid na Manchester City.

Kwa sasa Liverpool imekuwa ikimtumia Raheem Sterling kama mshambuliaji licha ya kuwepo kwa Mario Balotelli, Fabio Borini na Rickie Lambert kama washambuliaji asilia. 

Vile vile Liverpool wameonyesha nia ya kumnyakuwa mshambuliaji wa West Bromwinch Albion, Saido Berahino ambapo dau lake linatajwa kufikia Pauni 20M kutokana na mchezaji huyo kuonyesha kiwango kizuri na kufanikiwa kufunga mabao nane mpaka sasa.

Bado kocha wa Liverpool anaweza kuwa na mtihani mkubwa hasa ukizingatia kwamba, Daniel Sturridge ambaye anasubiriwa kwa hamu, amekuwa nje kwa miezi mingi na huenda atakaporejea ikamchukuwa muda kurudi kwenye ubora wake.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!