ROBERT PIRES ATOA YA MOYONI KUHUSU ARSENAL
Kigogo aliyestaafu wa Arsenal, Robert Pires, amehimiza klabu yake ya zamani kusajili mshambuliaji mpya iwe ndio mada kuu baada ya msimu huu kukamilika.
Pires alikuwa kigezo cha kikosi cha Gunners kilicho tawala ligi ya Premier ya Uingereza mapema mwongo uliopita na jina lake liliorodheshwa katika kumbukumbu za historia pale Arsenal walipokamilisha msimu wa 2003/04 bila kushindwa katika kampeni maarufu kama ‘Invincibles’.
Viungo wa sasa wa timu hiyo wameshindwa hata kunusia ufanisi wa watangulizi wao huku vijana wa mwalimu Arsene Wenger wakikamilisha miaka minane bila kushinda kikombe chochote.
Pires, ambaye ameshuhudia klabu yake pendwa ikishuka kutoka uongozi hadi nafasi ya nne katika mwendelezo wa mbio za Premier, anatumai Wenger atamsaini mshambuliaji ambaye atashirikiana na Olivier Giroud katika safu ya kusaka mabao.
“Ni muhimu sana kununua straika kwani unaweza kutumia mfumo wa 4-4-2 na hilo ndilo jambo muhimu zaidi kumtafuta msaidizi wa Giroud.
“Kwa sasa, msimu si mbaya. Wanamiliki nafasi ya nne na wanacheza dhidi ya Wigan kwenye semi fainali za kombe la FA. Ikiwa watashinda Manchester City wikendi hii, chochote chaweza kutendeka,” Pires alisema.
“Imani yangu imejikita kwa Arsene Wenger, kwa timu hii na wachezaji wenyewe,” aliongeza
0 comments:
Post a Comment