NIONAVYO MIMI: KWA SASA NAMBISHIA SIR ALEX FERGUSON.
Na Oscar Oscar Jr
+255789784858
Ni kweli mimi ni kijana ambaye ukipenda unaweza kuita wa kizazi cha Digital, ingawa Digital ya kizazi changu ni ile ya kutumia simu za Button na Antena na sio hiki cha Adroid ambacho kazi yake ni touch screen tu.
Najua namna ya kumsikiliza mtu mzima akiwa anaongea, najua namna ya kujenga hoja, najua kijizuia pale anaponikera na kubwa zaidi, najua namna ya kujpanga kumbishia bila hata kugombana naye.
Sir Alex Ferguson ni moja kati ya makocha wachache bora ambao kizazi changu cha Digital, nimepata kuwashuhudia. Ubingwa wa Ulaya alioutwaa mbele ya timu ya Bayern Munich mwaka 1999 na taji la ligi kuu Uingereza alilotwaa kwenye msimu wake wa mwisho, ni kumbukumbu ambayo siwezi kusahau kamwe.
Baada ya kustaafu kazi ya ukocha, Ferguson alitoa kitabu chake ambacho pamoja na mambo mengine, alimzungumzia kiungo wa Liverpool na timu ya taifa ya Uingereza, Jordan Henderson na kumponda kadri ya uwezo wake.
Ferguson ni mfalme wa Old Trafford, ni mfalme wa soka, ni mfalme pia wa EPL. Kumbishia anachosema, unapaswa kuwa umezaliwa zama za simu za Button na Antena au zile za kutumia Sanduku la Posta! Ferguson alisema Henderson ni mchezaji wakawaida sana na hajui namna ya kukimbia na mpira uwanjani na mengine mengi.
Nilitazama pambano la Liverpool dhidi ya Everton msimu huu nikiwa ndani ya Studio za BBC hapa Dar es Salaam na baada ya mechi, niliamua kutafuta takwimu za wachezaji wote wa mechi hiyo.
Henderson ndiye alikuwa amepiga pasi nyingi kuliko mchezaji yoyote wa Liverpool. Kwa upande wa viungo watatu wa kati, yeye alikuwa na pasi 65, Adam Lallana 40 huku mtu mzima Steven Gerrard, akiwa na pasi 35 pekee.
Watu wengi msimu uliopita hawakuipata nafasi Liverpool ya kufanya vizuri kwenye ligi kuu na mimi nikiwemo lakini, mwishoni mwa msimu Liverpool walitutoa nishai watu wengi tu. Naamini kuwa Henderson atakuja kuwatoa nishai watu wengi tu kasoro mimi pengine na Brendan Rodgers.
Baada ya kitabu hicho cha Ferguson wengi walitoa maoni yao na kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alisema kuna uwezekano Ferguson alianza kuandaa kitabu hicho kabla ya kustaafu. Nakubaliana na mzee Wenger, pengine Ferguson alianza kumuandika Henderson tangu alipokuwa klabu ya Sunderland.
Wakati Henderson ananunuliwa kutoka Sunderland, msimu huo alikuwa amepiga pasi za kwenda mbele kwa asilimia 38 pekee. Msimu uliopita akiwa na Liverpool ya Brendan Rodgers, alikuwa na asilimia 63.8 ya pasi zake zilizokwenda mbele. Nadhani Ferguson anamzungumzia Jordan Henderson yule wa Sunderland na sio huyu wa Rodgers.
Najua ni vigumu kwa kocha wa Man United kumsifia mchezaji wa Liverpool na kinyume chake na ndiyo maana, Ferguson hakumsifia hadi Steven Gerard lakini, ni vema kumueleza Ferguson kuwa msimu wa 2010/2011 Henderson akiwa Sunderland alipiga pasi zilizofika 1,334 na msimu uliopita akiwa na Liverpool, alipiga pasi zilizofika 2,007. Ferguson sio mbishi, atanielewa tu.
Henderson ni box to box Midfielder, aina ya viungo wanaojua kukaba, kutengeneza nafasi za kufunga na wao wenyewe kufunga. Ni aina ya kina Yaya Toure, Arturo Vidal na Aaron Ramsey. Kitu pekee anachokosa kwa sasa, ni uwezo wa kufunga magoli.
Msimu uliopita alifunga magoli manne pekee, bado ni machache mno ukilinganisha na kijana mwenzie wa Arsenal, Aaron Ramsey ambaye alifunga magoli 10 ya ligi kuu na kutengeneza pasi nane zilizozaa magoli.
Henderson anazidi kukua, ana zidi kuimarika. Nina imani kubwa na kijana huyu wa Anfield kufanya vizuri kama hatopata majeruhi ya kumuweka nje muda mrefu msimu huu.
Steven Gerrard alifunga magoli 13 msimu uliopita na kwa sababu jua liko machweo kwa upande wake, Henderson anatakiwa kuchukuwa jukumu hilo.
Ukitazama takwimu zake za tacles na Interceptions, unagundua kabisa kuna siku Rais wa Real Madrid Florentino Perez anaweza kutoa wallet yake na kutangaza dau la Pauni Milion 50 kumpeleka kijana Estadio Santiago Bernabeu.
0 comments:
Post a Comment