Na Chikoti Cico
Old Trafford patawaka moto siku ya “Boxing day” kwenye mfululizo wa mechi za ligi kuu nchini Uingereza ambapo wenyeji Manchester United wataialika timu ya Newcastle United kwenye mtanange huo unaotarajiwa kuwa wa piga nikupige.
Manchester United baada ya kushinda michezo sita mfululizo walitoka sare mchezo uliopita dhidi ya Aston Villa matokeo yaliyopelekea timu hiyo kuendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 32 nyuma ya Mancheter City na Chelsea.
Kocha wa Manchester United Louis van Gaal kuelekea mchezo huo atawakosa viungo Ander Herrera, Marouane Fellaini na Daley Blind ambao ni majeruhi.
Pia atawakosa mabeki Luke Shaw na Marcos Rojo ingawa mlinzi wa katikati Chris Smalling ambaye alikuwa majeruhi anatarajiwa kurejea kwenye mchezo huo dhidi ya Newcastle.
Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha mshambuliaji wa Manchester United, Robin van Persie amehusika kwenye magoli tisa dhidi ya Newcastle katika michezo nane iliyopita ya ligi huku akifunga magoli sita na kutoa pasi tatu za magoli (assist).
Kikosi cha Manchester United kinaweza kuwa hivi: De Gea, Jones, Smalling, Evans, Rafael, Carrick, Di Maria, Young, Mata, Rooney, Van Persie
Kwas upande wa Newcastle United baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya wapinzani wao wa jadi timu ya Sunderland kwa kufungwa kwa goli 1-0 matokeo yaliyopelekea timu hiyo kushika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 23 wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo kutafuta ushindi kwa nguvu zote ili kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi.
Kocha wa Newcastle Alan Pardew kuelekea mchezo huo atawakosa kiungo mkabaji Cheick Tiote ambaye amesimamishwa kucheza mchezo mmoja baada ya kuonyeshwa kadi ya tano ya njano kwenye mchezo dhidi ya Sunderland.
Pia kocha huyo atawakosa makipa Tim Krul na Rob Elliot ambao ni majeruhi, viungo Mehdi Abeid na Siem de Jong pamoja na kurejea mazoezini pia watakosekana kwenye mchezo huo sambamba na Rolando Aarons, Gabriel Obertan na Ryan Taylor ambao ni majeruhi.
Kwa upande wa Newcastle kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha wamekuwa na rekodi mbaya kwa mechi za “Boxing day” ugenini huku wakiwa wamecheza michezo tisa na kushinda mchezo mmoja tu huku wakifungwa michezo sita na kutoka sare michezo miwili.
Kikosi cha Newcastle United kinaweza kuwa hivi: Alnwick, Janmaat, Taylor, Coloccini, Dummett, Williamson, Colback, Gouffran, Sissoko, Cisse, Perez
0 comments:
Post a Comment