Searching...
Image and video hosting by TinyPic
28 December 2014
Sunday, December 28, 2014

Uchambuzi: Yanga vs Azam


Ndani ya uwanja wa Taifa  leo utapigwa mchezo mmoja ambao unazikutanisha timu zinazolingana pointi, Yanga vs Azam kwenye muendelezo wa ligi kuu Tanzania bara mzunguko wa nane. 


 Na Oscar Oscar Jr

Yanga tayari wamepoteza michezo miwili msimu huu na kushinda mechi nne huku wakitoka sare mara moja. Kwa upande wa Azam ambao tayari wamejikusanyia alama 13, wamepoteza mechi mbili pia msimu huu huku wakipata ushindi mara nne na kutoka sare mara moja. 

Bado wataendelea kuwakosa Joseph Kimwaga, Frank Domayo huku pamoja na kuanza mazoezi mepesi, bado kuna hatihati ya kumkosa pia nahodha wa timu hiyo, John Bocco ambaye amekuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Ukitazama safu ya ulinzi ya Yanga kuelekea mchezo wa leo, tayari watamkosa nahodha wao, Nadir Haroub na kuna uwezekano mkubwa wa Mbuyu Twite na Kelvin Yondani kuanza kama walinzi wa kati. 

Tayari Yanga imeruhusu magoli matano mpaka sasa na ubora wa safu ya ushambuliaji ya Azam, inaonyesha dalili za kuutikisa ukuta wa kocha Hans Van Der Pluijm.

Azam ambao walikuwa nchini Uganda, wamefanikiwa kucheza mechi nne na kuambulia ushindi mmoja tu kwenye mechi zao za kirafiki huku wakiwa wamefunga mabao matano tu na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara saba katika ziara hiyo. 

Kuelekea mchezo wa leo, kuna uwezekano mkubwa wa mfungaji bora wa Azam wa msimu uliopita, Kipre Tchetche na Didier Kavumbagu kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza na hivyo kuwasumbua walinzi wa Yanga

Azam wanaonekana kuwa na tatizo kubwa kwa upande wa safu ya Ulinzi ambapo bado hakuna maelewano mazuri baina ya Agrey Morris, Pascal Wawa na Golikipa, Mwadini Ally

Kwenye mechi ambazo wamecheza pamoja za kirafiki, wamekuwa watu wanaoruhusu mabao mepesi na leo huenda langoni akaanza Aishi Manula badala ya Mwadini Ally.

Ukitazama safu ya ushambuliaji ya Yanga ambayo imefunga mabao tisa mpaka sasa, unagundua kuwa imeongezewa nguvu kwa usajili wa Kpah Sherman na Amis Tambwe. 

Kama kocha wa Yanga atamrudisha Mrisho Ngassa kucheza kama winga huku Simoni Msuva akipewa nafasi ya kurejea kwenye kikosi cha kwanza, Azam watakuwa na kazi kubwa ya kuwazuia watu hao kutokana na kasi waliyonayo hasa wanapotokea pembeni.

Kiungo Mudathir Yahya ni moja ya wachezaji wa safu ya Kiungo wa Azam ambao wamekuja kwa kasi kubwa sana. Ukirejea kwenye mchezo wa kirafiki baina ya Azam na Mtibwa Sugar, utagundua kuwa, Mudathir alikuwa nyota wa mchezo. 


Ana nguvu, pasi zake ni za uhakika na hata namna anavyocheza kwa kushirikiana na Amri Kiemba wanaifanya timu itengeneze muunganiko mzuri kati ya kiungo na safu ya ushambuliaji.

Yanga wanapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo kutokana na historia ya timu hizi zinapokutana lakini, ukitazama namna timu zilivyotengenezwa kiufundi, Azam wanaonekana kukaa pamoja na benchi lao la ufundi kwa muda sasa na wanaweza kutumia kigezo hicho kuiadhibu Yanga kwenye mchezo wa leo.

Tatizo kubwa la timu ya Yanga linaonekana kwenye safu ya kiungo mahali ambapo baada ya kuondoka kwa Chuji na Domayo, bado hapajapatiwa ufumbuzi. 

Hassan Dilunga, Nizar Khalfan na Haruna Ninyonzima ni baadhi ya wachezaji ambao kuna uwezekano wa kuanza kwenye eneo hilo kuelekea mchezo wa leo.

Bado matumaini makubwa ya Yanga yataendelea kumtazama Simon Msuva ambaye ndiye mfungaji bora wa timu hiyo mpaka sasa akiwa na mabao matatu huku kwa upande wa Azam licha ya uwepo wa Kipre Tchetche bado Mshambuliaji Didier Kavumbangu mwenye mabao manne anaweza kuwa mwiba mchungu kwa wana Jangwani hao.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!