REAL MADRID YAENDELEA KUCHEZEA VITASA.
Matumaini ya Real Madrid kutwaa ubingwa wa ligi ya Uhispania, La Liga, yalipata pigo kubwa baada ya kuchakazwa 2-1 na Seville huku wapinzani wao wakuu, viongozi Atletico Madrid na Barcelona wakitamba katika mechi za Jumatano.
Mshambuliaji wa Colombia, Carlos Bacca, alifunga magoli mawili kuwapa wenyeji ushindi wao wa sita mfululizo baada ya mchezaji bora duniani, Cristiano Ronaldo, kufungua uongozi.
Majirani na waasimu wao, Atletico walifungua mwanya wa alama tatu na Real baada ya kuwapiku Granada 1-0 huku Barca, ambao waliangusha watanashari wao 4-3 kwenye kivumbi cha El Clasico Jumapili, kusonga hadi nafasi ya pili na ushindi wa 3-0 dhidi ya Celta Vigo uwanjani Camp Nou.
Barca, ambao walifaidika na mabao mawili kutoka nyota chipukizi wa Brazil, Neymar, wako alama moja nyuma ya Atletico.
Real walijitosa uwanjani na nia ya kuinuka mara moja baada ya kupoteza mechi ya kwanza kwa 32 walichocheza awali mikononi mwa Barca na walianza mechi yao ugenini Seville kwa kishindo huku Gareth Bale na Karim Benzema wakikosa nafasi wazi za kufunga.
Ilichukua dakika 14 kwa staa wao Ronaldo kufungua udhia kupitia mkwaju wa adhabu ambao ulibadilishwa mwendo na kutua wavuni na mlinda ngome Ivan Rakitic huku kipa wa Seville, Beto, akitizama bila kujua la kufanya.
Dakika nne baadaye, Bacca alitia ndani baada ya mashabulizi makali pale alipounganishiwa na straika mwenzake Jose Antonio Reyes aliyemwandalia pasi mwanana.
Ikisalia dakika 18, shambulizi la kushitukiza lilinasa Real pale Rakitic alipotimuka hadi eneo la wapinzani wao, kumchenga Pepe na kumlisha Bacca boli na mshambuliaji huyo hakupoteza muda na kufungua mkwaju ulioishia wavuni.
Hatima ya mabingwa wa ligi hiyo Barca, ambao wataialika Atletico katika mechi ya kufunga msimu, iko mikononi mwao baada ya kuwaelemea Celta Vigo.
Neymar alifungua orodha ya mabao kabla ya golikipa wao mashuhuri, Victor Valdes, kujeruhiwa vibaya goti lake akidaka mpira na kulazimika kuondolewa uwanjani na machela.
Lionel Messi aliendeleza ustadi wake mbele ya lango kwa kufunga la pili dakika ya 30 kabla ya Neymar kukamilisha ushindi huo na bao lake la pili ikisalia 23 mechi kukatika.
Bila shaka, Diego Costa, mshambuliaji matata wa Atletico, ndiye aliyepata la ushindi nyumbani kwao Vincente Calderon dhidi ya Granada katika mechi ngumu.
0 comments:
Post a Comment