Na Chikoti Cico
Moja ya mechi kubwa kabisa nchini Hispania na duniani kote wikendi hii ni mechi kati ya Real Madrid dhidi ya Barcelona itakayopigwa kwenye uwanja wa Bernabeu.
Hii ni mechi ambayo huvuta hisia za wapenzi wengi wa soka duniani huku sababu kubwa ikiwa ni katika mechi hii maarufu kama el clasico ndipo wachezaji wawili bora duniani Christiano Ronaldo na Lionel Messi wanapokutana.
Real Madrid wanaoishika nafasi ya tatu wakiwa na alama 18 kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Hispania maarufu kama la liga, wanaingia kwenye mechi hii wakihitaji kushinda ili kupunguza tofauti ya alama nne dhidi ya vinara Barcelona ambao wanaongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na alama 22.
Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti anatarajia kumkosa kiungo Gareth Bale ambaye ni majeruhi huku beki Sergio Ramos akitarajiwa kurejea uwanjani baada ya kukosekana kwenye mechi iliyopita ya ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool kutokana na kuwa majeruhi.
Mshambuliaji wa Real Madrid Christiano Ronaldo ambaye mpaka sasa ana magoli 15 kati ya mechi saba alizoichezea Real Madrid msimu huu anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu ya Real Madrid.
Mfungaji bora wa kombe la Dunia, James Rodriguez aliyesajiliwa kutoka Monaco ambaye atakuwa anacheza kwa mara ya kwanza kwenye mechi hii ya el clasico.
Kikosi cha Real Madrid kinaweza kuwa hivi: Casillas; Carvajal, Pepe, Varane, Marcelo; Kroos, Modric; James, Isco, Ronaldo, Benzema
Kwa upande wa Barcelona, kocha Luis Enrique anatarajia kuendeleza rekodi nzuri ya kutokufungwa hata mechi moja toka kuanza kwa ligi nchini Hispania.
Matokeo ambayo yameifanya Barcelona kuwa kileleni mwa msimamo wa la liga wakiwa na alama 22 huku wakishinda michezo saba na kutoka sare mchezo mmoja.
Mshambuliaji Luis Suarez aliyesajiliwa na Barcelona kutoka timu ya Liverpool na ambaye alikuwa amefungiwa na FIFA kutokujihusisha na soka kwa muda wa miezi minne baada ya kumg’ata beki wa Italia Giorgio Chiellini wakati wa kombe la Dunia, anatarajiwa kucheza kwenye mechi baada ya kumaliza kifungo hicho.
Mchezaji bora wa dunia mara nne Lionel Messi anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya timu ya Barcelona akishirikiana na Neymar katika kutafuta alama tatu muhimu dhidi ya wapinzani wao wa jadi.
Wakati huo huo, Messi anaweza kuifikia rekodi ya magoli 251 ya mfungaji bora wa muda wote kwenye ligi kuu ya Hispania Telmo Zarra kwani mpaka sasa Messi ana jumla ya magoli 250.
Kikosi cha Barcelona kinaweza kuwa hivi: Bravo; Alves, Pique, Mathieu, Alba; Busquets, Rakitic, Iniesta; Neymar, Messi, Suarez
0 comments:
Post a Comment