Searching...
Image and video hosting by TinyPic
23 October 2014
Thursday, October 23, 2014

Mkoa mzima wa Shinyanga unazizima na ujio wa Dar Young African




 Na Samuel Samuel, Shinyanga.

Mkoa mzima wa Shinyanga unazizima na ujio wa Dar Young African hasahasa hii manispaa ya Shinyanga palipo na dimba kongwe nchini la Kambarage. Uwanja uliojengwa mahususi kumuenzi baba wa taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere. 

Stand United waliopanda ligi msimu huu jumamosi hii, watakuwa wenyeji wa Dar Young African katika mtanange wa kusisimua . 

Mechi hii hapa mkoani Shinyanga imevuta hisia za watu wengi hasa wapenda soka. Viongozi wa Stand United kwa nyakati tofauti wamekaliliwa wakisema " tunajua mechi itakuwa ngumu sana ukizingatia Yanga ina uzoefu mkubwa katika ligi kuliko sisi lakini tutapigana kufa na kupona kuchukua pointi tatu. 

Tunafahamu Yanga ina wapenzi wengi sana mkoani hapa hali ambayo itawafanya washangiliwe sana lakini tunasisitiza wakazi wa mkoa huu, Stand United ndio timu inayowakilisha mkoa wao hivyo tunaomba mtupe sapoti kubwa hiyo jumamosi". 

Stand United ambayo zamani ilijulikana kama Scrapper FC imejichimbia katika uwanja wa Shycom ikijifua vilivyo kujiaandaa na mechi hiyo. Stand inakwenda kukutana na Yanga ikiwa na kumbu kumbu ya kutoka sare ya 0-0 na Kagera Sugar katika mechi iliyopigwa mjini Kagera. 

Yanga nao wanakwenda Shinyanga wakitoka kutoshana nguvu na mahasimu wao wakubwa Simba SC. Stand United inayonolewa na kocha Masawe mara nyingi inapokuwa uwanja wa nyumbani inatumia mfumo wa 4-4-2 na timu hiyo inasifika kwa pasi nyingi na kasi katika kushambulia. 

Yanga inayonolewa na Mbrazil Maximo isitegemee mtelemko katika tumu hii ingawa Stand wana kumbukumbu mbaya na uwanja huo baada ya kunyukwa 4-1 katika mechi ya ufunguzi na wageni wenzao katika ligi, Ndanda FC. 

Yanga inakwenda Shinyanga baada ya miaka mingi sana na hiyo ilitokana na mkoa huo kutokuwa na timu ligi kuu kwa kipindi kirefu toka iliposhuka daraja timu ya 82 Rangers. Kwa mara ya mwisho Yanga kucheza katika uwanja huo ilitoka sare ya 2-2 na 82 Rangers timu iliyokuwa ikimilikiwa na JWTZ. 

Maximo anahitaji sana ushindi katika mechi hiyo ili aiweke timu yake vizuri kisaikolojia. Yanga imekuwa na mwendo wa kusua sua ukilinganisha na aina ya usajili iliyofanya. 

Kama Yanga itaifunga Stand jumamosi, itakuwa imeamsha ari na kasi ya kuufukuzia ubingwa uliochini ya Azam FC.

 Baada ya mechi hii Yanga itaelekea mkoani Kagera kucheza na wana Nkulukumbi Kagera Sugar. " Nani kuibuka kidedea Jumamosi?!" Dakika 90 zitaamua.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!