Na Chikoti Cico
Kiungo wa West Ham United, Alex Song hivi karibuni ametangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Kameruni baada ya kutoitwa kwenye kikosi cha kocha wa Kameruni Volker Finke kuelekea michuano ya mataifa ya Afrika itakayofanyika nchini Equatorial Guinea kuanzia tarehe 17 Januari.
Taarifa za kustaafu kwa Song zimewashangaza mashabiki wengi wa soka barani Afrika hasa ukizingatia kwasasa Song yuko kwenye kiwango kizuri lakini pia katika umri wa miaka 27 bado angeweza kuwa msaada kwenye timu yake taifa ambayo inashiriki michuano hiyo ya AFCON.
Wachambuzi wa soka pia mashabiki na kila mdau wa soka la Afrika anaweza kusema lolote kuhusu uamuzi huo wa Song lakini ukiangalia kwa jicho la tatu utaona kabisa ni uamuzi ambao kwa sehemu kubwa una faida sana kwa kiungo huyo.
katika miaka zaidi ya mitatu iliyopita Song amekuwa na wakati mgumu kisoka hasa baada ya kuhama kutoka Arsenal na kwenda Barcelona usajili ambao uliinufaisha Arsenal zaidi kuliko Song mwenyewe ambaye muda mrefu alikaa benchi akisubiria Sergio Busquets aumie.
Hivyo kupelekwa kwa mkopo West Ham kutoka Barcelona ni kama kumefufua kiwango cha Song, mpaka sasa Song amekuwa sehemu ya wachezaji wenye msaada mkubwa kwa timu hiyo inayofundishwa na kocha Sam Allardyce.
Ingawa mpaka sasa West Ham inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi lakini ubora wa Song kwenye safu ya kiungo ya timu hiyo umeiwezesha timu hiyo maarufu kama “wagonga nyundo wa London” kupoteza michezo sita tu kati ya 20 mpaka sasa kwenye ligi.
Huku pia wakicheza mchezo ambao unawavutia mashabiki wa timu hiyo tofauti na msimu uliopita ambapo timu ilikuwa inatumia zaidi mipira mirefu mpaka kufikia hatua mashabiki walitaka kocha wa timu hiyo Sam Allardyce afukuzwe kazi.
Hivyo kustaafu kuichezea kameruni hii inamaanisha Song atakuwa na muda mrefu wa kuichezea West Ham bila ya kuwa na majukumu ya kucheza mechi za kimataifa ambazo wakati mwingine husababisha mchezaji kuumia na kupelekea kupokonywa namba kwenye klabu yake.
Na binafsi siushangai sana uamuzi wa Song kustaafu kuichezea timu ya taifa na kujikita zaidi kuichezea West Ham kwasababu huu ndiyo wakati mzuri wa Song kutengeneza pesa akiwa kwenye kiwango bora kabisa huku akicheza mahali ambapo anapendwa na kujaliwa.
Katika umri wa miaka 27 hii inamaanisha umri wa Song haurudi nyuma hivyo sitashangaa kwenye majira ya joto Song akisajiliwa na timu kubwa na kupokea mshahara mnono zaidi hasa kipindi hiki ambacho kiwango chake kipo juu na katika umri ambao bado ana nguvu za kuendana na mikikimikiki ya ligi mbalimbali duniani.
NAWASILISHA.
0 comments:
Post a Comment