Searching...
Image and video hosting by TinyPic
20 October 2014
Monday, October 20, 2014

Liverpool bado sana.


Na Oscar Oscar Jr

Ushindi wa jana wa Liverpool wa magoli 3-2 dhidi ya QPR bado haukutokana na ubora wa Liverpool. Magoli mawili ya kujifunga kutoka kwa Steven Caulker na Richard Dunne, yalichangia Liverpool kuibuka na alama tatu huku magoli mawili ya kijana wa QPR Eduardo Vargas, yakidhihirisha makosa yale yale ya walinzi wa Liverpool chini ya Brendan Rodgers.

Brendan Rodgers bado anatafuta mtu sahihi wa kucheza kwenye nafasi ya kiungo mkabaji lakini, kuna ishara kuwa bado hajapatikana. Jana alimuanzisha Emre Can huku Jordan Henderson na Steven Gerrard wakicheza kwa juu yake lakini alichemsha na baadae akatolewa na nafasi yake ikachukuliwa na Joe Allen.

Adam Lallana angalau jana alicheza vizuri lakini sio yule aliyekuwa Southampton na kitenda cha kumuacha nje Phillipe Coutinho, kingeweza kuigharimu Liverpool. 

Kuingia kwa kiungo huyo wa Brazil, kulibadilisha mchezo na kumfanya Raheem Sterling arejee nyuma ya mshambuliaji, mahali amabapo anaonekana kufanya vizuri sana kuliko pale anapotumiwa kama winga.

Bobby Zamora, Austin na Isla, walikuwa hatari sana mbele ya lango la liverpool huku kiungo Sandro akilitawala dimba. Baada ya kuumia na kutolewa kwa kiungo huyo wa QPR, Liverpool walionekana kupumua na kuanza kuimarika ingawa bado Balotelli aliendelea kuwa angusha.

Simon Mignolet pamoja na makosa yake ya kutocheza mipira ya krosi na kufanya uamuzi wa kuliacha lango pasipo stahili, jana alionekana kuwa shujaa baada ya kuokoa michomo mingi iliyopigwa na vijana wa kocha Harry Redknapp. Steven Gerrard pamoja na utu uzima wake, jana alifanya kazi nzuri sana.

Ukitazama takwimu za washambuliaji ambao wamepiga mashuti mengi langoni msimu huu, Mario Balotelli ana karibiana na kina Kun Aguero, Graziano Pelle na Diego Costa. Wakati hao wenzie wakikimbizana kwa ufungaji wa magoli, Balotelli bado hajafunga hata goli moja.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!