Searching...
Image and video hosting by TinyPic
16 November 2014
Sunday, November 16, 2014

Kuelekea mataifa ya Afrika 2015- Guinea ya Ikweta.


Na Oscar Oscar Jr

Timu ya Bafana Bafana jana waliweza kujikatia tiketi ya kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika ambayo imepangwa kufanyika Guinea ya Ikweta kufuatia ushindi wao wa magoli 2-1 dhidi ya timu ya Sudani kwenye mchezo uliopigwa jijini Durban, nchini Afrika ya Kusini.

Magoli ya timu ya Bafanabafana yalifungwa na Thulani Serero (38) na Tokelo Rantie (53) huku, Ibrahim Salah Mohamed akifunga kwa upande wa Sudan na kuwapatia bao la kufutia machozi.

Mechi hiyo ilikuwa na hisia kubwa kwa mashabiki na wachezaji kufuatia kuomboleza kifo cha aliyekuwa nahodha na golikipa wa timu hiyo, Senzo Meyiwa ambaye aliuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwezi uliopita.

Vinara hao wa kundi A, wameungana na mataifa mengine ambayo tayari yameshafuzu kwa michuano hiyo mikubwa barani Afrika. Mbali na Afrika Kusini, Algeria, Cape Verde na Tunisia, sambamba na wenyeji ambao wanafuzu moja kwa moja timu ya Equatorial Guinea, tayari wanasubiri timu nyingine zitakazo kamilisha idadi ya timu 16 ambazo zitawekwa kwenye makundi manne.

Bingwa mtetezi wa michuano hiyo, timu ya taifa ya Nigeria, jana waliweza kuweka hai matumaini yao ya kufuzu kwa michuano hiyo kwa ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Congo na sasa, watalazimika kushinda mchezo wao wa mwisho dhidi ya timu ya Afrika Kusini ambayo haijapoteza hata mchezo mmoja ili kuweza kujihakikishia nafasi.

Kwa upande wa Cameroon, wameonekana kurejea kwenye ubora wao na kusahau machungu yote waliopitia kwenye kombe la dunia na mpaka sasa hawajapoteza mchezo hata moja. 

Jana walifanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya timu ya Jamhuri ya watu wa Congo wa bao 1-0. Timu ya Taifa ya Ivory Coast, ambao waliifunga Sierra Leone 5-1 siku ya Ijumaa, nao wako kwenye wakati mzuri wa kufuzu kwa michuano hiyo ya Afrika.

Goli pekee lililofungwa na mshambuliaji wa Stoke City ya Uingereza na raia wa Senegal, Mame Biram Diouf, lilitosha kufuta ndoto za mabingwa wa 2010 wa Afrika, timu ya Misri kufuzu kwa michuano hiyo baada ya mchezo kumalizika huku Farao wakilala kwa bao 1-0.

Siku ya Ijumaa, timu ya Tunisia ilikwenda sare na timu ya taifa ya Botswana lakini bado Senegal wanaongoza kundi hilo. Upande mwingine, Burkina Faso na Gabon wote wakifuzu jana jumamosi huku Burkina Faso walishinda 1-0 mbele ya Lesotho wakati Gabon wakipata pointi moja baada ya kutoka sare ya 0-0 dhidi ya Angola.

Mabingwa wa Afrika 2012, timu ya taifa ya Zambia, nayo iliweza kujihakikishia nafasi ya kushiriki kwenye michuano hiyo mara baada ya kuibamiza Mozambique bao 1-0. Cape Verde, ambao wameshafuzu, walipata ushindi wa 3-1 dhidi ya  Niger na kuongoza kundi F.
 
Kundi E bado halitabiriki kwa sababu kila timu ina nafasi ya kwenda au kuzikosa fainali hizo na hii ni mara baada ya timu ya taifa ya Uganda kuifunga Ghana bao 1-0 huku Guinea wakiifunga Togo bao 4-1. 

Ghana wanaongoza kundi wakiwa na alama nane wakati, Uganda na Guinea ambao watakutana siku ya Jumanne kila mmoja akiwa na alama saba na Togo ambao wanashika mkia, wana pointi sita na kama watamfunga Ghana, bado wana nafasi ya kufuzu kwa michuano hiyo.

Malawi walifanikiwa kupata ushindi wa bao 2-0 mbele ya Mali huku mchezo mwingine ukiishuhudia Algeria wakiizamisha Ethiopia kwa mabao 3-1 mchezo uliopigwa jana Jumamosi. 

Algeria tayari wameshafuzu huku mmoja kati ya Malawi na Mali ndiye atakayefuzu na kwenda Guinea ya Ikweta kwa fainali hizo.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!