Koeman na Pelle wanyakua tuzo za mwezi wa tisa ligi kuu ya Uingereza.
Na Chikoti Cico
Tuzo za kocha bora na mchezaji bora wa mwezi kwenye ligi kuu ya Uingereza zote zimekwenda kwa timu ya Southampton, hii ni baada ya kujikusanyia alama 9 kati ya mechi tatu walizocheza zilizowawezeshwa kuwa nafasi ya pili nyuma ya Chelsea kwa mwezi wa tisa.
Kocha wa Southampton Ronald Koeman amechukua tuzo ya kocha bora wa mwezi wa tisa mbele ya kocha wa Chelsea Jose Mourinho, kocha wa Leicester City Nigel Pearson na kocha wa Crystal Palace Neil Warnock ambao wote walikuwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo hiyo.
Wakati kocha wa Soton akiibuka kidedea katika tuzo hiyo pia mshambuliaji Graziano Pelle naye aliibuka kidedea kwenye tuzo ya mchezaji bora wa mwezi wa tisa baada ya kufunga magoli matatu ndani ya mwezi wa tisa huku mawili akifunga dhidi ya Newcastle United na lingine moja dhidi ya QPR.
Southampton iliyoanza ligi vizuri kwasasa ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu ya Uingereza ikiwa na alama 13 nyuma ya Machester City yenye alama na 14 na vinara wa ligi hiyo Chelsea wenye alama 19.
Kocha wa Southampton akihojiwa na waandishi wa habari baada ya kushinda tuzo hiyo alisema “Tumekuwa na mwanzo mzuri wa msimu na kwa hilo ni vizuri kushinda, ni tuzo binafsi lakini tunajua tulifanya pamoja”
Kocha huyo kutoka Uholanzi aliendelea kusema “Unahitaji wachezaji ambao wana ari na malengo na najivunia wachezaji wangu kwa tulivyoanza msimu ila lazima tuendelee”
Pelle aliyehamia Southampton akitokea Feyenoord ya Uholanzi akiongea na waandishi wa habari baada ya kunyakuwa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi wa tisa hiyo alisema;.
“ nilipokuja hapa, mwanzoni mwa mwezi haikuwa rahisi, kulikuwa na tofauti na changamoto kubwa hivyo ilinibidi kufanya juhudi zaidi ya kawaida”
Akaendelea kusema “kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi wa tisa ni hisia kubwa, nahitaji kumshukuru mwalimu kwa kunipa nafasi ya kuja hapa”
0 comments:
Post a Comment