Yaya Toure aibeba Manchester City dhidi ya Swansea City.
Na Oscar Oscar Jr
Baada ya kusemwa vibaya na vyombo mbalimbali vya Habari nchini Uingereza na Ulaya kwa ujumla, Kiungo wa kimataifa wa Ivory Coast, Yaya Toure amenza kuwaziba midomo wote waliodhani mchezaji huyo ameshuka kiwango na kumnyima heshima anayostahili pale alipofunga bao zuri kwenye ushindi wa bao 2-1 dhidi ya timu ya Swansea hapo jana kwenye dimba la Etihad.
Yaya Toure ambaye alifunga magoli 20 ya ligi kuu nchini Uingereza msimu uliopita na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara mbili ndani ya miaka mitatu, msimu huu alianza kwa kusua sua huku akishindwa kuibeba timu hiyo hasa pale ilipokuwa kwenye wakati mgumu.
Yaya Toure ambaye pia amefanikiwa kuisaidia nchi yake ya Ivory Coast kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika ambazo zinatarajia kuanza kutimua vumbi mwezi Januari mwakani, alikuwa nguzo pia kwenye mchezo wao wa mwisho pale walipokutana na wababe wenzao wa Afrika, timu ya Cameroon na kwenda suluhu pacha.
Kocha Manchester City, Manuel Pellegrini hakusita kumwagia sifa kiungo huyo baada ya mchezo wa jana na kudai kuwa, atafanya makubwa pia msimu huu.
Manchester City baada ya ushindi huo, wanaendelea kuwa nyuma ya vinara wa ligi hiyo timu ya Chelsea kwa tofauti ya alama nne.
Manchester City ambayo bado inaendelea kumkosa kiungo David Silva na mshambuliaji, Eden Dzeko ambao ni majeruhi, jana walishuhudia ujio wa nahodha wa timu hiyo, Vincent Kompany ambaye alikosa mechi kadhaa kutokana na majeruhi huku ukuta wa Martin Demichelis na Eliaquim Mangala ukionyesha mapungufu makubwa mno.
Manchester City Jumanne hii watakuwa na kibarua kigumu pale watakapo wakaribisha wababe wa Bundesliga, timu ya Bayern Munich kwenye dimba la Etihad kwenye mchezo wa klabu bingwa Ulaya ambao Manchester City wanatakiwa kupata ushindi ili kuweka matumaini yao hai ya kufuzu kwa hatua ya 16 bora.
Swansea City walikuwa wa kwanza kujipatia bao kutokana na mchezo mzuri wa Nathan Dyer ambaye alimpasia Wilfred Bonny na kuweka mpira wavuni huku, mshambuliaji wa Manchester City, Steven Jovetic akisawazisha baada ya gonga gonga nyingi za vijana wa Pellegrini.
Baadaye, Yaya Toure alipokea pasi ya kisigino kutoka kwa Fernandinho na kupiga kwa ustadi mkubwa mpira uliomshinda kipa wa Swansea, Lukas Fabianski na kuwapa The Citizens bao la ushindi.
0 comments:
Post a Comment