Searching...
Image and video hosting by TinyPic
1 December 2014
Monday, December 01, 2014

FIFA Ballon d’Or wabakia watatu.


Na Chikoti Cico

Baada ya wachezaji 23 kutajwa kugombania tuzo ya mchezaji bora wa dunia ijulikanayo kama FIFA Ballon d’Or hatimaye wamechujwa na kubakia wachezaji watatu ambao ni Christiano Ronaldo, Lionel Messi na Manuel Neuer.

Ronaldo mwenye miaka 29 ambaye kwasasa ndiye anayeshikilia tuzo hiyo anapewa nafasi kubwa ya kunyakua tena kwa mara ya tatu baada ya kuchukua mwaka 2008 na 2013.

Hii ni kutokana na kuwa na msimu mzuri wa mwaka 2014 huku mpaka sasa akiwa amefunga magoli 50 katika mechi 46 alizoichezea Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno.

Wakati huo huo nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno alisaidia Madrid kuchukua kombe la ligi ya mabingwa Ulaya, kombe la Mfalme (Copa del Ray) na UEFA Super cup huku pia akishikilia rekodi ya kufunga magoli mengi kwasasa kwenye historia ya kombe la Ulaya maarufu kama “EURO”.

Lionel Messi naye pia anapewa nafasi ya kuchukua tena tuzo hiyo kwa mara ya tano baada ya kuinyakua mara nne mfululizo kuanzia mwaka 2009-2012.

 Messi mwenye umri wa miaka 27 karibuni ameweza kuvunja na kuweka rekodi mpya kwenye ligi ya mabingwa Ulaya na ligi kuu nchini Hispania maarufu kama la liga.

Kwenye ligi ya mabingwa Ulaya Messi amefikisha magoli 74 na kuwa mfungaji bora wa muda wote akivunja rekodi ya Raul Gonzalez ya magoli 71.

Pia amefikisha magoli 253 na kuwa mfungaji bora wa la liga kwa muda wote huku akiivunja rekodi iliyowekwa na Telmo Zara ya magoli 251.

Aliisaidia Argentina kufika fainali ya kombe la Dunia na kuibuka mchezaji bora wa michuano hiyo iliyofanyika nchini Brazili mapema mwezi wa saba.

Wakati Ronaldo na Messi wakipambana kwa rekodi za magoli kuelekea tuzo hiyo, kipa wa timu ya taifa ya Ujerumani na Bayern Munich Manuel Neuer mwenye miaka 28 amekuwa kipa wa kwanza kuwepo kwenye listi ya wachezaji watatu toka kipa wa zamani wa Ujerumani na Bayern Oliver Khan kufanya hivyo mwaka 2002.

Neuer ambaye aliibuka kipa bora wa michuano ya kombe la Dunia iliyofanyika Brazili huku akiisaidia Ujerumani kunyakua kombe hilo baada ya kuifunga Argentina kwa goli 1-0.

Pia akiisaidia Bayern Munich kuchukua makombe mawili nchini Ujerumnai naye anapewa nafasi ya kuchukua tuzo hiyo lakini akipata upinzani mkubwa toka kwa Messi na Ronaldo.

Pia kwenye upande wa tuzo ya kocha bora, yupo kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Low, kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti na Diego Simeone aliyeiongoza Atletico Madrid kunyakuwa kombe la ligi kuu na kuifikisha timu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Washindi wa tuzo hizo watatangazwa Januari 12 kwenye hafla itakayofanyika jijini Zurich nchini Uswisi yalipo makazi ya shirikisho la soka Duniani FIFA.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!