Bayern hakamatiki Bundesliga
Na Oscar Oscar Jr
Mabingwa wa Ujerumani, timu ya Bayern Munich ambao bado hawajapoteza mchezo wowote msimu huu, waliendeleza kampeni yao ya kusaka taji la Bundesliga, kwa kuitandika timu ya Hoffenheim kwa mabao 4-0 Jumamosi na kuzidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kuu.
Timu iliyokuwa inakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Ujerumani, VfL Wolfsburg walijikuta wakichezea kichapo cha bao 3-2 ugenini dhidi ya timu ya Schalke 04.
Kwa matokeo hayo, Bayern sasa wana mwanya wa alama saba kileleni, huku wakiwa hawajapoteza mchezo wowote kwenye mashindano matatu wanayoshiriki msimu huu.
Mario Goetze alifunga kutoka umbali wa hatua 23 kupitia shuti la kwanza la Bayern lililolenga goli dakika ya 23. Mchezaji wa kimataifa wa Poland, Robert Lewandowski akafunga kwa kichwa bao lake la sita msimu huu baada ya krosi murua kutoka kwa Arjen Robben.
Roben naye aliongeza bao la tatu dakika za mwishoni za mechi, kabla ya nguvu mpya, Sebastian Rode kufunga la mwisho dakika tatu kabla ya mechi kumalizika baada ya kupokea mpira kutoka kwa Bastian Schweinsteiger.
Schweinsteiger aliingia kama nguvu mpya na kucheza mara yake ya kwanza tangu fainali ya Kombe la Dunia baada yake kupona jeraha la goti. Bayern sasa wana alama 30.
Hoffenheim walimaliza na wachezaji 10 baada ya Adam Szalai kulambwa kadi nyekundu dakika za lala salama za mchezo huo.
0 comments:
Post a Comment