Na Chikoti Cico
Nyasi za uwanja wa Anfield zitaikaribisha Sunderland kumenyana na Liverpool katika moja ya mechi za ligi kuu nchini Uingereza, mchezo utakaopigwa saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, na utasimamiwa na refa, Neil Swarbrick.
Liverpool wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na mfululizo wa ushindi kwenye mechi mbili zilizopita dhidi ya Stoke City na Leicester City hivyo kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers anatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo akiwa na ujasiri wa kutafuta alama tatu nyingine hivyo kuendelea kusogea juu kwenye msimamo wa ligi.
Huku mchezo wa ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Basel ukiwa njiani, Brendan anaweza kuwapumzisha wachezaji wachache kama Nahodha Steven Gerrard, Glen Johnson, Lucas Leiva, Raheem Sterling na Rickie Lambert na nafasi kuchukuliwa na Alberto Moreno, Emre Can na Fabio Borini.
Ikijikusanyia alama 20 na kushika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi kuelekea mchezo huo dhidi ya Sunderland, Liverpool itawakosa Daniel Sturridge, Mario Balotelli, Mamadou Sakho, Suso na Jon Flanagan ambao ni majeruhi.
Wakati huo huo, takwimu kuelekea mchezo huo zinaonyesha rekodi nzuri ya Liverpool dhidi ya Sunderland. Katika michezo tisa iliyopita ya ligi kuu, Liverpool ameshinda michezo mitano, wakitoka sare michezo mitatu na kufungwa mchezo mmoja.
Kikosi cha Liverpool kinaweza kuwa hivi: Mignolet; Manquillo, Skrtel, Toure, Moreno; Allen, Can, Henderson; Coutinho; Lallana, Borini
Kwa upande wa timu ya Sunderland baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Manchester City kwa kufungwa magoli 4-1, kocha wa timu hiyo, Gus Poyet anatarajiwa kuingia kwenye mchezo dhidi ya Liverpool kupigana kufa na kupona kupata matokeo mazuri ugenini, mpaka sasa Sunderland inashika nafasi ya 14 ikiwa na alama 14 kwenye msimamo wa ligi.
Adam Johnson na Wes Brown ambao walikosekana kwenye mchezo dhidi ya Manchester City, wanatarajiwa kurejea kikosini kuivaa Liverpool wakati huo huo mlinzi Sebastian Coates hatacheza mchezo huo kwasababu yuko kwa mkopo Sunderland akitokea Liverpool.
Kikosi cha Sunderland kinaweza kuwa hivi: Pantilimon; Vergini, O'Shea, Brown, Reveillere; Cattermole, Rodwell, Larsson; WIckham, Alvarez, Fletcher
Sunderland wanaonekana kuwa na rekodi mbovu dhidi ya Liverpool Anfield kwani katika michezo 15 iliyopita ya ligi kuu, Sunderland wamefungwa michezo nane na kutoka sare michezo 7 huku wakiwa hawajashinda mchezo hata mmoja.
0 comments:
Post a Comment