Searching...
Image and video hosting by TinyPic
21 November 2014
Friday, November 21, 2014

Simba inamahitaji mengine kuliko saini ya Juma Kaseja.


Na Samuel Samuel

Klabu ya soka ya Simba yenye masikani yake mitaa ya msimbazi , Kariakoo jijini Dar Es Salaam ipo nafasi ya nane katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi tisa baada ya kutoka sare michezo sita na kushinda mchezo mmoja dhidi ya Ruvu shooting. 

Timu hiyo inayonolewa na kocha Mzambia, Patrick Phiri kwa nyakati tofauti viongozi wake wamekuwa wakinukuliwa na vyombo vya habari kutaka kumrejesha kwenye himaya yao golikipa nguli nchini, Juma Kaseja. 

Golikipa huyo kwa sasa anakipiga na mahasimu wao wakubwa nchini, klabu ya Dar Young African . Simba wamefikia hatua hiyo kutokana na golikipa huyo kutofurahi maisha ndani ya Yanga kutokana na kukosa nafasi ya kucheza na sintofahamu juu ya kumaliziwa pesa zake za mkataba . 

Simba kama klabu kiufundi inahitaji saini ya Kaseja? " Simba inayoundwa na damu changa golini tena wenye vipaji kama Manyika Jr. na Casilasi chini ya mkongwe Ivo Mapunda sidhani kama wanahitaji saini ya Kaseja. 

Simba ilimwacha Kaseja kwa kulaumiwa kushuka kiwango na baada ya hapo Yanga ilimsajili Kaseja ambaye mpaka leo amekosa namba ya kudumu ndani ya kikosi cha Yanga baada ya golikipa namba moja wa timu hiyo " Dida" kusimama imara. 

Hii inaonesha kiufundi bado Kaseja hajarudi kwenye kiwango chake kilichomfanya arithishwe mikoba ya timu ya taifa baada ya Peter Manyika kustaafu. Mbali na hapo klabu ya Simba haina tatizo la kipa baada ya kijana wa miaka 18 Manyika Jr kuonesha uwezo mkubwa golini. 

Simba inahitaji Umoja wa viongozi ili kuvunja makundi ndani ya klabu hiyo. Mpaka ligi inasimama kundi la Simba UKAWA limekuwa likilalamikiwa kuihujumu timu hiyo achilia mbali Wambura na watu wake. 

Kiufundi bado Simba ina tatizo la beki wa kati na beki wa kulia. Bado Isihaka , Tshabalala hawajaimarika vizuri kudumu vyema dakika 90 za mchezo wakiwa katika ubora wao. Ni muda wa klabu hiyo ya msimbazi kununua beki mmoja mwenye uzoefu.

Unapomsimamisha Kiemba, Kisiga na kutaka kuwaachia Azam kumchukua Ndemla mbadala wake ndo Kaseja? Mnahitajika kutulia hapa kuliko kuifikiria saini ya Kaseja.

Kabla hamjamleta Kaseja, fikirieni ustawi wa kipaji cha Manyika Jr. Kaseja kaiandikia barua Yanga kuvunja mkataba wake moja ya sababu yake ni kukosa namba ndani ya kikosi cha Maximo.

Maana yake ni kwamba, ili kumsajili mchezaji huyo ni lazima apate nafasi ya kucheza kitendo ambacho kitamfanya Manyika awe chaguo la tatu ama la NNE. 

Nadhani muda wa Simba kuachana na Kasseja na badala yake wanapaswa kuangalia mapungufu yao kwenye idara tofauti za kiufundi na kuondoa mkanganyiko kwenye Uongozi.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!