Searching...
Image and video hosting by TinyPic
18 November 2014
Tuesday, November 18, 2014

Kufuzu Mataifa ya Afrika leo.


Na Oscar Oscar Jr

Hatimaye mechi za mwisho za kutafuta tiketi ya kufuzu kwa michuano ya Maifa ya Afrika, inatarajia kutimua vumbi siku ya Jumatano ya leo.

Mabingwa watetezi Nigeria watakuwa miongoni mwa miamba wengine wakiwemo mabingwa mara nne wa kombe hilo, Ghana na Ivory Coast watakaokuwa wakipigana kufa au kupona siku ya Jumatano kufuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika mwakani  nchini Equatorial Guinea. 

Super Eagles walifufua kampeni yao wikendi iliyopita mjini Pointe-Noire, walipowalaza wenyeji Congo kwa bao 1-0 na kufuta kichapo cha kushangaza cha 3-2 nyumbani Septemba. 

Nigeria, walio nafasi ya pili Kundi A na alama saba kutokana na mechi tano, watajipanga kuwafunga vinara wa kundi hilo timu ya Bafana bafana ya nchini Afrika Kusini katika uwanja mpya wa kimataifa wa Akwa Ibom, mjini Uyo ili kupata nafasi ya kufuzu kwa michuano hiyo barani Afrika. 


Kocha wa Nigeria, Stephen Keshi, ambaye atakuwa bila kiungo wa kati wa Reading, Hope Akpan aliyeumia begani wakiwa Congo, watalazimika kufanya kila wawezalo kuweza kupata alama hizo tatu na kufuzu mbele ya Bafana bafana.

Mabingwa wa mwaka 1996, Afrika Kusini hawajafungwa katika mechi tano za kufuzu chini ya kocha Ephraim 'Shakes' Mashaba lakini watasafiri hadi jiji la kusini la Uyo wakiwa na ushindi mmoja pekee kwenye mechi kumi walizocheza dhidi ya Nigeria.
Nigeria na Afrika Kuisni zilitoka sare tasa mjini Cape Town Septemba. 


Congo walio nambari tatu kwenye msimamo wa kundi, wanatumai Afrika Kusini wanaweza kuwafaa sana kwa kuikosesha ushindi  Nigeria huku wao wakishinda mechi yao dhidi ya Sudan. 

Congo, waliocheza katika fainali hizo mara ya mwisho miaka 14 iliyopita, wanaweza pia kufuzu kama timu bora  nambari tatu, iwapo watashinda dhidi ya Sudan huku Guinea, wakiilaza timu ya  Uganda nyumbani. 

Black Stars, timu ya Ghana walichezea kichapo cha 1-0 wakiwa Uganda Jumamosi, lakini bado wanaongoza Kundi E na alama nane na watahitaji sare tu dhidi ya wageni Togo mjini Tamale kufuzu.

Jordan Ayew aliyekuwa amesimamishwa kucheza atarejea, lakini kakake mkubwa, Andre Ayew aliumia paja kule Uganda na huenda asicheze. 

Guinea walifungua wazi Kundi E baada yao kuwatandika Togo 4-1 mjini Lome wikendi iliyopita, na sasa wanahitaji kuwafunga Uganda kwa zaidi ya 2-0 mechi yao ya mwisho nyumbani ili kujikatia tiketi.
Uganda na Guinea sasa wana alama saba, lakini Uganda wako mbele kwa kufuata kanuni ya ubabe wakati timu hizo zilipokutana ambapo, Uganda walishinda kwa bao 2-0 Jijini Kampala, mwezi Septemba.

Vita nyingine itakuwa kati ya Ivory Coast na DR Congo kupigania nafasi iliyosalia ya kufuzu moja kwa moja katika Kundi D baada ya bao la kipindi cha pili la Vincent Aboubakar dhidi ya DRC mjini Yaounde, kuwapa Indomitable Lions uongozi thabiti wa alama 13.
Ivory Coast wana alama tisa, tatu mbele ya DRC, na sasa wanahitaji angalau sare nyumbani Abidjan dhidi ya Cameroon kujihakikishia nafasi yao. 

Ndovu hao, ambao sasa nahodha wao ni Yaya Toure wa Manchester City, walifungwa 4-2 nchini Cameroon miezi mitatu iliyopita katika pambano la kukata na shoka. 

Mali, Malawi na Ethiopia nao watapigania tiketi nyingine isiyo na mwenyewe Kundi B, ambapo tayari kiongozi wake ni Algeria.
Mali wana pointi sita na watakaribisha Algeria mjini Bamako, nao Malawi, ambao pia wana alama sita lakini wanapungukiwa na mabao, watacheza na Ethiopia wanaoshika mkia kundini na alama tatu. 

Mali wanahitaji ushindi dhidi ya Algeria, walio na rekodi bora baada ya mechi tano, kufuzu. 

Hata Ethiopia wanaoshika mkia bado wana nafasi ya kufuzu endapo watashinda dhidi ya Malawi kwa zaidi ya mabao mawili huku wakiomba timu ya Mali ifungwe dhidi ya Algeria. 

Malawi pia wanaweza kufuzu wakiwalaza Ethiopia kwa mabao mengi baada yao kuwalaza 3-2 nyumbani Septemba. Watapanda hadi alama tisa na kuwaondoa Mali kwa kigezo cha mshindi wakati timu hizo zilipokutana ambapo Mali alifungwa 2-0 mjini Bamako. .

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!