Arsenal njia nyeupe kuelekea 16 Bora Ulaya.
Na Chikoti Cico.
Arsenal haoo 16 bora. Timu ya Arsenal imefanikiwa kuingia hatua ya 16 bora baada ya kushinda kwa magoli 2-0 dhidi ya Borrusia Dortmund mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Emirates.
Timu hiyo kutoka London iliweza kupata goli la kuongoza mapema kabisa kwenye dakika ya pili, goli lililofungwa na Yaya Sanogo kabla ya Alex Sanchez kuongeza goli la pili dakika ya 57 na kuifanya Arsenal kuondoka uwanjani kifua mbele.
Goli la Sanchez la dakika ya 57 liliihakikishia Arsenal kuingia hatua ya 16 bora ya michuano ya ligi ya mabingwa huku likiwa ni goli lake la 13 katika michezo 16 aliyoichezea Arsenal tokea aliposajiliwa kutoka Barcelona.
Kwa mara ya 15 mfululizo kocha wa Arsenal Arsene Wenger ameiwezesha timu hiyo kufika hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Ulaya ingawa bado Arsenal hawajawahi kunyakua kombe hilo, ila huwezi kubeza rekodi hiyo ya Wenger.
Kwa kushinda mchezo huo dhidi ya Borrusia Dortmund Arsenal wamefikisha alama 10 katika michezo 5 ya ligi ya mabingwa Ulaya huku wakishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi D nyuma ya vinara Dortmund wanaoongoza kundi hilo wakiwa na alama 12.
Kocha wa Dortmund Jurgen Klopp ambaye amekuwa akihusishwa kuifundisha Arsenal baada ya kuondoka kwa Wenger huku akionekana kukerwa na matokeo ya mchezo huo.
Akiongea na waandishi wa habari baada ya mchezo huo alisema “ Kulikuwa na wakati na wasaa ambapo tulifanya tulichotaka kufanya lakini vipindi hivyo vilikuwa vichache sana, muda mwingi hatukuwa bora na Arsenal walikuwa washindi waliostahili usiku huu, ni basi hatukuwa bora vya kutosha”.
0 comments:
Post a Comment