Searching...
Image and video hosting by TinyPic
3 August 2014
Sunday, August 03, 2014

Uchambuzi Mechi ya Msumbiji vs Tanzania

Na Oscar Oscar Jr

Taifa Stars leo itakuwa dimbani ugenini dhidi ya timu ya taifa ya Msumbiji kuwania nafasi ya kusonga mbele na kutinga kwenye makundi ya mchujo kueleke AFCON 2015 ambapo mchezo uliopita ulimalizika kwa timu hizo kufungana mabao 2-2. 

Ili Stars iweze kusonga mbele, inahitaji kupata ushindi leo wa aina yoyote au sare itakayoanzia mabao matatu. Inawezekana? pengine hili ni swali gumu kujibika lakini soka ni mchezo usiotabirika.

Tatizo kubwa la Stars linaanzia kwenye safu ya kiungo ambapo kwenye siku za hivi karibuni, Mwinyi Kazimoto na Erasto Nyoni wamekuwa wakianza kutokana na majeruhi yanayowaandama Frank Domayo na Jonas Mkude. 

Mwinyi kazimoto bado anaonekana kutokuwa kwenye ubora wake, fundi wa kupiga mashuti, pasi za uhakika na uwezo wa kuiunganisha timu vyote kwa mechi za hivi karibu hajavionyesha. Erasto Nyoni yuko kwenye majukumu mapya ya kiungo mkabaji, bado hajaonyesha kiwango cha kuitendea haki nafasi hiyo.

Kwa mfumo wa 4-3-3 ambao umekuwa ukipendwa na kocha Marts Nooij, bado walinzi wa Stars wa pembeni hawaonekani kuisaidia timu kupandisha mashambulizi hasa pale timu inapokuwa inamiliki mpira. Oscar Joshua na Shomary Kapombe bado wameonekana kuendelea kubaki nyuma hata kama timu inashambulia.

Stars inaonekana kuimarika kwenye safu ya ushambuliaji na hii inadhihirishwa na mabao mannne ambayo waliyafunga kwenye mechi mbili zilizopita. Walipata mabao mawili ugenini dhidi ya Zimbabwe na mengine mawili mbele ya Msumbiji nyumbani. 

Mbwana Samatta anaweza kuonekana kama hajaonyesha makali yake kama wengi wanavyotarajia lakini tatizo pekee ni kumkosa kiungo wa kumtengea mipira kwenye njia kitu ambacho kimekuwa kikimlazimu ashuke chini na kupokea mipira toka kwa walinzi wake.

Bado walinzi wa Stars wa kati, haonekani kuimarika. Canavaro anaweza kuonekana bora lakini ukweli ni kwamba, bado sio mzuri hasa anapokutana na mshambuliaji mjanja uso kwa uso. 

Kitu kinachombeba Nadil ni nguvu na namna anavyoweza kucheza mipira ya juu hasa krosi. Yondani ni beki mzuri shida yake ni kukosa mbinu mbadala tu ya kumdhibiti adui hasa anapomtoka kitu ambacho kina mfanya kucheza rafu nyingi dimbani.

Mrisho Ngassa ni moja kati ya wachezaji bora kabisa ingawa kwa mechi za karibuni ameonekana kucheza chini ya kiwango, kocha anaweza kumpumzisha na kumuanzisha ama Mcha au Msuva ili kuimarisha winga zetu na pia kama Yondani ataonekana kutokuwa kwenye ubora, mabadiliko ya kumuingiza Agrey Moris yasisubiri mpaka timu ifungwe.

Bado Stars inahitaji kujilinda zaidi kuliko kushambulia hasa kwenye kipindi cha kwanza ili kuepuka kufungwa bao la mapema. Msumbiji ni timu yenye rekodi nzuri sana ya kutuondoa mashaindanoni hasa haya ya kuelekea AFCON, hivyo watataka kuendeleza rekodi yao. 

Msumbiji wanaonekana pia ni timu inayocheza kwa kuhitaji matoa. Baada ya kuwafunga kwao Sudan bao 5-0, walihitaji sare tu Ugenini na wakafanikiwa. Walipokuja kwetu utaona kabisa lengo lao ilikuwa ni sare na bao la ugenini na wakafanikiwa.

Ukitazama mchezo wao wa awali na Stars, utagundua kuwa walijaza viungo wanne dhidi ya wa kwetu wawili kitu amabacho kiliwafanya kutawala dimba. Kama na leo watafanya hivyo kwenye mfumo wao wa 4-4-2 ni lazima mawinga wetu wawe wanarudi ndani kukaba pindi Stars inapokuwa imepoteza mpira ili kwenda sambamba na kasi ya viungo wao.

Kwa mchezo wa leo msumbiji wana nafasi kubwa ya kusonga mbele kwa sababu sare ya bila kufungana au ile ya 1-1 inatosha kuwavusha lakini, Stars nao wana nafasi kwa sababu ushindi hata wa bao 1-0 utaweza kuwafanya wasonge mbele.

Mungu Ibariki Tanzania, kila la kheri Stars.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!