Searching...
Image and video hosting by TinyPic
3 November 2014
Monday, November 03, 2014

Uchambuzi: Real Madrid vs Liverpool


Na Chikoti Cico

Ligi ya mabingwa Ulaya inatarajiwa kurejea tena wiki hii kwa mechi za raundi ya pili huku mechi inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka, ni mchezo kati ya Real Madrid dhidi ya Liverpool utakaopigwa siku ya Jumanne saa 4:45 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu, jijini Madrid.

Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti anatarajia kuingia kwenye mchezo huo kutafuta alama tatu muhimu zitakazowawezesha kuvuka ngazi ya makundi na kuingia kwenye hatua mtoano kwani mpaka sasa Madrid wanaongoza kundi B wakiwa na alama tisa baada ya kushinda mecho zote tatu za raundi ya kwanza.

Baada ya kukosekana kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Liverpool ambao Madrid walishinda kwa magoli 3-0 na pia kwenye mchezo dhidi ya Barcelona kutokana na kuwa majeruhi, kiungo mwenye kasi Gareth Bale anatarajiwa kurejea tena uwanjani kuikabili Liverpool hapo Jumanne.

Kikosi cha Real Madrid kinaweza kuwa hivi: Casillas; Carvjal, Pepe, Ramos, Marcelo; Modric, Kroos; Rodriguez, Bale, Ronaldo; Benzema

Beki ya Liverpool ambayo mpaka sasa imeruhusu magoli 21 kwenye mashindano yote, watakuwa na kazi ya kuzuia safu ya ushambuliaji ya Madrid itakayoongozwa na Christiano Ronaldo ambaye mpaka sasa ana magoli 20 katika mecho zote Madrid alizocheza toka kuanza kwa msimu huu.

Baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa jumla ya magoli 3-0 kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers ana kibarua kigumu mbele ya Madrid ingawa Liverpool wanahitajika kupigana kufa na kupona kuweza kupata matokeo mazuri ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kuweza kuvuka kwenye hatua ya makundi.

Liverpool ambao mpaka sasa wanashika nafasi ya pili sawa na Ludogorets kwenye msimamo wa kundi B wote wakiwa na alama tatu kati ya michezo mitatu ya raundi ya kwanza, wataingia kwenye mchezo huo huku wakiendelea kumkosa mshambuliaji Daniel Sturridge hivyo Brendan anatarajiwa kumwanzisha Mario Balotelli kuongoza safu ya ushambuliaji ya Liverpool.

Wakati huo huo safu ya ushambuliaji ya Liverpool, bado inatia shaka kwani takwimu zinaonyesha mpaka sasa wachezaji waliofunga magoli mengi ni viungo Steven Gerrard na Raheem Sterling ambao kila mmoja ana magoli matatu huku Balotelli akifatia akiwa na magoli mawili.

Kikosi cha Liverpool kinaweza kuwa hivi: Mignolet; Johnson, Skrtel, Lovren, Moreno; Gerrard, Lallana; Henderson, Coutinho, Sterling; Balotelli

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!