Na Chikoti Cico
Timu ya Real Madrid baada ya kupoteza mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Valencia kwa kufungwa magoli 2-1, wamekubali kuchezea tena kichapo kwenye mchezo wa kwanza wa kombe la Mfalme dhidi ya wapinzani wao wa jadi timu ya Atletico Madrid kwa kufungwa magoli 2-0.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye uwanja wa Vicente Calderon nyumbani kwa Atletico Madrid, magoli yote mawili ya timu hiyo inayofundishwa na Diego Simeone yalipatikana kipindi cha pili kupitia kwa Raul Garcia dakika ya 58 kwa njia ya penati na Jose Gimenez kwenye dakika ya 76 akiunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu.
Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Fernando Torres alicheza mchezo huo ukiwa ni mchezo wake wa kwanza toka asajiliwe kwa mkopo kutoka AC Milan na kwa mara ya kwanza akiwa mchezaji wa Atletico timu yake iliweza kupata ushindi.
Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti ambaye hakumwanzisha Christiano Ronaldo ambaye anasumbuliwa na goti kwenye mchezo huo na kuja kumwingiza kipindi cha pili atakuwa na mlima mrefu wa kuupanda kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu tarehe 15, Alhamisi ya wiki ijayo.
0 comments:
Post a Comment