Sure Boy kupewa tuzo leo Azam Complex
Na Oscar Oscar Jr
Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Azam, Abubakary Salumu maarufu kwa jina la "Sure Boy", leo anatarajia kukabidhiwa tuzo yake.
Shirikisho la soka Tanzania limejenga utamaduni wa kutoa tuzo kwa mchezaji bora wa kila mechi na baadae, huchagua mchezaji bora wa mwezi.
Wataalamu hao waliowekwa na TFF, mwezi Octoba walimchagua kiungo huyo wa timu ya Azam kuwa mchezaji bora wa mwezi na anatarajia kupokea tuzo hiyo leo ambapo timu yake itakuwa ikicheza na Coastal Union mchezo wa ligi kuu Tanzania bara kwenye uwanja wa Azam Complex.
Azam ambao wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu baada ya kujikusanyia pointi 10, wamejikuta katika wakati mgumu baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo na leo, wanataka kurudisha hali ya kujiamini kwa kusaka ushindi mbele ya timu ya Coastal Union.
Coastal Union wanashika nafasi ya pili baada ya kukusanya alama 11 nyuma ya timu ya Mtibwa Sugar ambao wana alama 14. Safu ya ushambuliaji ya Coastal Union tayari imefunga mabao nane na leo watakuwa na mtihani mgumu wa kuipenya ngome ya Azam ambayo inaundwa na wachezaji kama Agrey Moris wenye uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi.
Wakati huo huo pia, shirikisho la soka Tanzania wametangaza kuwa, dirisha dogo la usajili litafunguliwa rasmi tarehe 15 Novemba na linatarajiwa kufungwa, tarehe 15 Desemba.
0 comments:
Post a Comment