Na Chikoti Cico
Timu za taifa za Mali na Guinea ambazo zimelingana alama na magoli ya kufunga na kufungwa kwenye msimamo wa kundi D wa kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kutoka sare ya goli 1-1 kwenye mchezo wa mwisho wa kundi hilo zinasubiria droo ya kamati ya shirikisho la soka la Afrika (CAF) kuamua timu ipi itaingia hatua ya robo fainali.
Katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Estadio de Mongomo ulishuhudia timu hizo mbili zikitoka sare ya goli 1-1 huku Guinea wakiwa wa kwanza kupata goli kwenye dakika ya 15 ya kipindi cha kwanza kupitia kwa Kevin Constant kabla ya Mali kusawazisha kwenye dakika ya 47 ya kipindi cha pili kupitia kwa Modibo Maiga.
Kutokana na matokeo hayo timu zote mbili zimefikisha alama tatu huku pia zikiwa na tofauti sawa ya magoli ya kufunga na kufungwa kitu ambacho kinapelekea Ibara ya 74 ya shirikisho la soka la Afrika (CAF) kutumika kuamua timu itakayosonga mbele kwenye hatua ya robo fainali. Sheria hiyo pia hutumiwa na shirikisho la soka Duniani (FIFA).
Baada ya mchezo huo taarifa kutoka CAF zilisema “katika kutumika kwa ibara ya 74 ya kanuni ya kombe la Mataifa ya Afrika, droo ya kubahatisha itafanyika kujua timu ya pili kwenye kundi D kati ya Mali ama Guinea”.
“Droo itafanyika wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya kombe la Mataifa ya Afrika Alhamisi tarehe 29 Januari 2015 saa 10 kamili kwa muda wa Guinea kwenye hoteli ya Hilton Malabo”.
Wakati huo huo mashabiki mbalimbali wa soka walitaka timu hizo mbili zipigiane penati kuamua timu itakayofuzu hatua ya robo fainali ikiaminika kwamba penati zitakuwa na burudani zaidi kuliko droo ambayo ni kama kucheza bahati nasibu. Kitu ambacho hakitaweza kutokea kutokana na Ibara hiyo ya 74 inavyoonyesha.
0 comments:
Post a Comment