Na Chikoti Cico
Timu ya taifa ya Ivory Coast imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuifunga timu ya taifa ya Kameruni kwa goli 1-0 kwenye mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Estadio de Malabo nchini Guinea ya Ikweta.
Mchezo huo ambao uliwakutanisha timu vigogo wa Afrika uliamuliwa kwa goli la Max Gradel kwenye dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza kwa shuti kali la mguu wa kulia. Goli lililoihakikishia Ivory Coast kuvuka hatua ya makundi.
Kwa matokeo hayo timu ya Ivory Coast maarufu kama “tembo” wamefuzu kwa hatua ya robo fainali baada ya kufikisha alama tano na kuongoza kwenye msimamo wa kundi D huku timu ya Kameruni ikiyaaga michuano hiyo baada ya kumaliza ikiwa na alama mbili mkiani mwa kundi D.
Kwenye hatua ya robo fainali Ivory Coast watakutana na Algeria siku ya Jumapili mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Estadio de Malabo. Wakati huo huo ushindi huo wa Ivory Coast unamaanisha wachezaji wa Manchester City Yaya Toure na Wilfried Bony hawatakuwepo kwenye mchezo wa ligi kuu nchini Uingereza dhidi ya Chelsea siku ya Jumamosi kitu ambacho inawezekana hakitawafurahisha mashabiki wa klabu hiyo
0 comments:
Post a Comment