Na Chikoti Cico
Klabu ya Barcelona imetinga hatua ya nusu fainali ya kombe la Mfalme (Copa del Rey) baada ya kuichapa Atletico Madrid kwa jumla ya magoli 4-2 baada ya michezo miwili ya robo fainali.
Barcelona ambayo ilishinda kwa goli 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali uliofanyika kwenye uwanja wa Camp Nou ilifanikiwa kushinda tena jana usiku kwa magoli 3-2 kwenye mchezo wa pili wa robo fainali uliofanyika kwenye uwanja wa Vicente Calderon.
Mchezo huo ambao ulitawaliwa na vituko vingi ikiwemo kiungo wa Atletico Madrid Arda Turan kumrushia kiatu mshika kibendera huku pia nahodha wa Atletico Gabi kupewa kadi nyekundu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kumtukana mwamuzi wa mchezo huo na Jordi Alba kudondoshwa na kibendera cha mwamuzi.
Ulishuhudia magoli mawili ya Neymar kwenye dakika ya 9 na 41 pamoja na goli la kujifunga la beki wa Atletico Miranda kwenye dakika ya 38 yakiihakikishia Barcelona nafasi ya kuingia nusu fainali ya Copa del Rey.
Magoli mawili ya Atletico kwenye mchezo huo yalifungwa na Fernando Torres kwenye dakika ya 1 ya mchezo na Raul Garcia kwenye dakika ya 30 kwa njia ya penati. Hivyo mpaka mwisho wa mchezo walikuwa ni Barcelona waliotoka kifua mbele na kufanikiwa kufuzu kwa hatua ya robo fainali.
0 comments:
Post a Comment