Searching...
Image and video hosting by TinyPic
29 January 2015
Thursday, January 29, 2015

Makala: Diego Costa “shetani” anayependwa Chelsea.

Na Chikoti Cico

“Mtaani palikuwa shuleni kwangu, uwanjani nilipigana na kila mtu, sikuweza kujizuia peke yangu. Nilimtukana kila mtu, sikuwa na heshima kwa wapinzani, nilidhani nilitakiwa kuwaua”. Hayo ni maneno kutoka kinywani kwa mshambuliaji wa klabu ya Chelsea, Diego Costa.
Ni maneno machache lakini yanakupa taswira ya kwamba Costa ni mchezaji wa aina gani, huyu sio mchezaji ambaye alipitia kwenye shule bora za soka (academy) na kufundishwa jinsi ya kucheza ama kuwaheshimu wachezaji wengine achilia mbali namna ya kufunga magoli, karibu kila kitu unachokiona kwa Costa leo hii kimetoka mtaani.
Siku chache baada ya nusu fainali ya pili ya kombe la Capita One dhidi ya Liverpool Costa yuko matatani baada ya kushtakiwa na chama cha soka nchini Uingereza (FA) kwa kosa la kumkanyaga Emre Can huku pia kwenye mchezo huo Costa alionekana kumkanyaga Skrtel na kusukumana na Gerrard na tayari amefungiwa michezo mitatu.
Huyo ndiye Costa ambaye haikumchukua muda mrefu kuizoea ligi ya Uingereza toka asajiliwe na klabu ya Chelsea kwenye majira ya joto akitokea klabu ya Atletico Madrid, ligi hiyo inayojulikana kwa matumizi makubwa ya nguvu mchezoni imeendana kabisa na Costa ambaye aina yake ya mchezo ni matumizi makubwa ya nguvu pia na mabavu katika kutafuta magoli.
Pamoja na vurugu na kila aina ya ubaya wa Costa lakini bado ni mshambuliaji tegemeo kwa klabu ya Chelsea ambaye mpaka sasa ameisadia klabu hiyo kuongoza kwenye msimamo wa ligi ya Uingereza ikiwa na alama 52 huku Costa akiifungia klabu hiyo jumla ya magoli 17 na hivyo kuongoza kwenye chati ya wafungaji bora nchini humo.
Inawezekana Costa akawa mshambuliaji mwenye roho mbaya na hata kumfananisha na “shetani” kutokana na mchezo wake wa vurugu lakini mbele ya kocha wa Chelsea Jose Mourinho Costa anabaki kuwa “malaika” asiye na “hatia” na hata baada ya kumkanyaga Emre Can tukio ambalo lilionekana kuwa wazi kabisa, Mourinho alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema “ni bahati mbaya”.
Kocha wa Chelsea Jose Mourinho wakati flani akimwongelea Costa baada ya kumsajili alisema “ hakuna aliyempa Costa chochote bure, kila mara ilibidi apigane sana….. haogopi chochote, yuko tayari kwa kila kitu” na hivyo ndivyo shule ya mtaani ilivyomfundisha Costa.
Mpaka sasa mshambuliaji huyo ameshaonyeshwa kadi nane za njano kwenye ligi kuu nchini Uingereza lakini kama alivyosema Mourinho “haogopi chochote, yuko tayari kwa kila kitu” hizo kadi za njano sio kitu kwake ilimradi baada ya dakika 90 za mchezo amefunga goli na kuipa timu yake ya Chelsea ushindi.
Mwisho nimalizie kwa maneno haya ya kiungo wa Chelsea Eden Hazard alipokuwa anamwongelea Costa alisema “unapocheza na mtu huyu inabidi ujitoea kwa kila kitu, unaweza kuona kwa kila kitendo kwa kila mpira anayatoa maisha yake. Hata kama asipofunga anayatoa maisha yake kwaajili yetu kwaajili ya wachezaji unapocheza naye ni kitu kizuri”.
Huyo ndiye Diego Costa mchezaji ambaye ungependa awepo kwenye klabu yako ili uwe salama dhidi yake kinyume cha hapo yatakukuta kama ya Emre Can na Martin Skrtle na wala “haogopi chochote,” na “yuko tayari kwa lolote”.
NAWASILISHA.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!