Searching...
Image and video hosting by TinyPic
30 December 2014
Tuesday, December 30, 2014

Natamani kumtazama tena Pascal Wawa dimbani.



 Na Samuel Samuel

Beki mpya wa kimataifa wa Ivory Coast na Azam, Paschal Wawa alicheza mchezo wake wa kwanza wa ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Yanga huku akionekana kuhemeshwa vya kutosha na washambuliaji wa wana Jangwani kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 anatakiwa kukaza buti zake.

Tanzania ni nchi ambayo hata Lionel Messi anaweza kufukuzwa, ni mahali ambapo mtu kama Christiano Ronaldo angeweza kupelekwa benchi kwa kile kinachoitwa kucheza chini ya kiwango kwenye mechi moja.

Hakuna anayeweza kukataa uwezo wa beki huyo wa zamani wa timu El-Merreikh, ukitazama umbo lake ni lazima utakubali tu. Ukitazama namna anavyojua kucheza mipira ya juu na kuondosha hatari, ni wazi utamkubali. 

Ni mwepesi na ana nguvu za kupambana kwa dakika zote 90 lakini timu zetu huwa haziangalii hayo yote. Ukimtazama namna alivyocheza kwenye mechi za kirafiki kule Uganda, ni wazi kuwa utakubaliana na mimi kuwa bado Wawa hajaweza kuwa katika ubora aliouonyesha kwenye kombe la Kagame kule nchini Rwanda.

Beki huyu aliyesimama kama beki namba nne akishirikiana na Aggrey Morris aliyesimama kama sentahafu alikumbuna na moto makali wa Dar Young African. Pongezi kwake Aggrey Morris na Erasto Nyoni ambao kwa namna moja walikuwa wakisahisha makosa yake. 

Wawa alionekana kukosa mbinu za ziada kuwahimili Amisi Tambwe na Kpah Sherman . walipokea mpira wanavyotaka na kuilazimisha beki ya Azam kuwa chini yao mara nyingi kurudi nyuma. 

Kukosa umakini wa mafowadi Yanga kuliwanyima ushindi. Wawa alionesha uwezo wa wastani hasa kuzuia washambuliaji wa kati kupokea mipira mizuri ndani ya adui. Ukitazama goli alilofunga Tambwe kwa free header Wawa, Himidi Mao, Kapombe na Aggrey wote walimwacha Tambwe aruke juu huru. 

Ukitazama mofoloji ya umbo la Wawa si wa kushindwa kutumia mwili wake. Makosa hayo almanusura Hussein Javu aandike bao la ushindi dakika ya 90. Kilicho mchanganya Wawa ni kasi ya mawinga wa Yanga na upokeaji mzuri wa mipira kwa washambuliaji wa kati. 

Msuva kushoto na Mrwanda kulia baadaye alitoka na kuingia Javu. Wawa anahitaji kazi ya ziada ili kujiweka sawa kuwamudu washambuliaji wajanja na wenye kasi kama Tambwe, Ngasa, Kpah, na hata wakikutana na Mtibwa Sugar wakae macho kwa mshambuliaji kama Ame Ally.

Ni mapema mno kuanza kutilia mashaka uwezo wa beki huyo lakini historia na utamaduni wa ligi na klabu zetu ndiyo unanifanya nimpe muda tena Wawa ili kuona kama atarudi kwenye ubora wake na kuisaidia Azam kutetea ubingwa wake na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!