Omega kuonyesha ubora ndani ya Sokoine?
Na Samuel Samuel
0652464525
Msimu wa 2013-14 wa ligi kuu Tanzania bara ukiitazama Tanzania Prisons mzunguko wa kwanza wa ligi kuu iliyumba na kujikuta ikipoteza au kutoa droo michezo mingi. Kocha mzoefu mwenye umbo kubwa David Mwamwanya alirekebisha mfumo wake wa kujilinda na kushambulia.
Kule mbele akaanza kumtumia Michael Peter na dimba la kati akimwamini sana Omega Seme mchezaji aliyempata kwa mkopo toka Yanga. Seme mwenye uwezo mzuri wa kutawala kiungo cha chini aliiwezesha timu hiyo kujinusuru kushuka daraja.
Omega alimchezesha vizuri Michael Peter ambaye aliibuka mfungaji mzuri wa timu hiyo. Kiwango cha kiungo huyo kiliwafanya Yanga kumrudisha kundini hasa baada ya kuondokewa na mafundi wao kama Frank Domayo na Athuman Chuji.
Kocha Mbrazili Marcio Maximo hakumpa sana nafasi kiungo huyo na kujikuta akimtumia kama mchezaji wa akiba kwa Mbuyu Twite na wakati mwingine alimwingiza kama beki wa kushoto akihitaji beki inayomiliki mpira na kupandisha timu kwa kasi.
Kukosa nafasi ya kucheza ndani ya Yanga, msimu huu wa dirisha dogo mchezaji huyo ametimkia Ndanda FC kwa mkopo. Jumapili hii wakazi wa Mbeya na mashabiki wa Dar young Africans watamuona Omega Seme ndani ya jezi za Ndanda FC akimiliki Dimba la kati dhidi ya Mbeya City.
Maboss wa Ndanda chini ya udhamini mnono wa Binslum Tyres hawakukosea kuinasa saini ya kiungo huyo mwenye sifa moja kubwa, kutoa pasi nzuri za mwisho na fundi wa kuanzisha mashambulizi makali ya pembeni.
Ndanda wasisite kumpanga Seme mechi ya jumapili kwa sababu uwanja wa sokoine na Mbeya City anavijua vizuri toka akiwa Tanzania Prisons.
Swali letu je, Omega Seme atang'ara katika kibarua chake cha kwanza dhidi ya Mbeya City timu inayosaka ushindi kwa udi na uvumba ? Mbeya City inaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi kuu huku Ndanda nao wakiwafuatia kwa kushika nafasi ya 13.
0 comments:
Post a Comment