Hiki ndicho kitakachomtesa Sserunkuma pale Simba.
Na Samuel Samuel
- 0652464525
Ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2013-14 ulishuhudia mchezaji wa kigeni toka nchini Burundi, Amis Tambwe akiibuka mfungaji bora kwa kutupia kwenye kamba magoli 19 huku mzawa Mrisho Ngasa akiwa na magoli 13.
Kama una kumbukumbu nzuri msimu wa 2012-13 pia mgeni Kipre Tchetche wa Azam FC aliibuka mfungaji bora na hata sasa Didier Kavumbagu kutoka nchini Burundi katika mechi Saba ana magoli manne na kuwa miongoni mwa vinara wa mabao kwenye VPL.
Tambwe kabla ya kutua Msimbazi, huko kwao alikotoka alikuwa mfungaji bora na hapa akaibuka pia mfungaji bora. Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kujipanga na kuipatia timu yake magoli mengi na muhimu.
Alipotua Simba kocha Abdallah Kibadeni na baadaye Mcoratia, Logarusic, walitengeneza mfumo ambao timu nzima kimashambulizi ilimpa msaada mkubwa mchezaji huyo kucheka na nyavu.
Tambwe akageuka mfalme ndani ya Simba. Hata viongozi na mashabiki wa timu hiyo wakampa saikolojia nzuri mchezaji huyo kwa kumuamini na kumuonesha mapenzi ya wazi wazi. Mara ligi ikaisha na Simba SC kuishia nafasi ya nne.
Usajili wa July Emanuel Okwi akatua Simba SC. Mganda huyo ana historia nzuri na klabu hiyo, ghafla upepo ukaanza kubadilika kwa Tambwe . Kocha mpya ndani ya Simba SC akaanza kuitengeneza timu kupitia mgongo wa Okwi.
Viongozi na mashabiki wakamsahau shujaa wao . Tambwe akaanza kuiona jehanamu ya soka ndani ya timu aliyoitumikia kwa mapenzi yote. Mwisho wa siku akatimkia zake Jangwani masaa machache kabla ya dirisho dogo la usajili kufungwa.
Simba SC si kwamba hawaikuiona thamani ya Tambwe baada ya ujio wa Okwi, bali usajili wa mwamba mwingine toka nchini Uganda Sserunkuma.
Mchezaji huyo amedumu na timu ya Gor Mahia nchini Kenya na mara mbili mfululizo ameiwezesha timu hiyo kuweza kutwaa ubingwa wa ligi kuu huku akiibuka mfungaji bora msimu uliopita.
Sserunkuma pia amewahi kuwa mchezaji bora wa mwaka nchini Kenya tukio ambalo halijawahi kutokea kwa miaka ya hivi karibuni kwa tuzo hiyo kuchukuliwa na mchezaji ambaye si raia wa Kenya.
Swali la kujiuliza kama ilivyo ada kwa wana Msimbazi hao, watamfanya Sserunkuma mfalme wa Simba kama ilivyokuwa kwa Okwi na Tambwe ?
Pili Sserunkuma ataweza kuvivaa viatu vya Tambwe kama mshambuliaji wa kati aliyewapa Simba SC magoli 19?! Sserunkuma ni lazima atambue nyota yake ipo katika mguu wake na kichwa chake kwa sasa bado Simba SC ipo na Emanuel Okwi ili ajenge jina ni lazima avivae viatu vya Tambwe.
0 comments:
Post a Comment