Haruna Chanongo kutambulishwa Kifalme huko Shinyanga.
Na Oscar Oscar Jr
Timu ya Stand United kutoka mkoani Shinyanga maarufu kama Chama la wana, jana ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye dimba la Ally Hassan Mwinyi pale Tabora dhidi ya timu ya Rinho Rangers.
Katika mchezo huo, Haruna Chanongo ambaye amegeuka kuwa kipenzi cha mashabiki wa Stand United alikuwemo na kuonyesha kiwango kizuri sana huku akifunga bao moja kati ya matatu yaliyofungwa.
Timu hiyo bado iko mkoani Tabaro na leo inashuka dimbani tena majira ya saa 10:30 kumenyana na Polis Tabora mchezo utakaopigwa pia kwenye dimba la Ally Hassan Mwinyi.
Baada ya mchezo huo Stand United watarejea mkoani Shinyanga ambako wamepanga kucheza mchezo mmoja wa kirafiki na majirani zao Mwadui Fc kwa lengo la kutambulisha wachezaji wao waliosajili kipindi cha dirisha dogo.
Stand United na Mwadui Fc ni timu zinazotoka mkoa mmoja na zinapokutana mara nyingi mchezo huo huteka hisia za wapenzi wengi wa soka wa mkoa huo. Stand United inasadikiwa kuongoza kwa mashabiki lakini Mwadui Fc ndiyo timu yenye kipato kikubwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii moja kwa moja kutoka mkoani Tabora, mwalimu wa Stand United, Bilal amesema vijana wake wako kwenye hali nzuri na wamejiandaa kuhakikisha wanafanya vema.
Stand United ambao wanashika nafasi ya 10, wanavaana kwenye mzunguko wa nane na vinara wa ligi kuu ya Tanzania bara, Mtibwa Sugar tarehe 27 kwenye dimba la Manungu kule mkoani Morogoro.
0 comments:
Post a Comment