Kumbe Okwi kalamba Milioni 58?
Mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda na klabu ya Simba, Emmanuel Okwi imeelezwa kuwa amelamba Milioni 58 kwenye usajili wake wa mwaka mmoja uliofanyika hivi karibuni baada ya mechi ya Mtani Jembe dhidi ya Yanga kumalizika kwa timu hiyo kushinda mabao 2-0.
Okwi ambaye alijiunga na timu hiyo akitokea klabu ya Yanga, ameonekana kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho cha kocha Patrick Phiri na amehusika kwa asilimia zaidi ya 90 kwenye magoli saba ya ligi kuu ambayo yamefungwa na Simba hadi sasa.
Kiwango chake bora kiliwashawishi viongozi wa klabu hiyo kumpatia nyongeza ya mkataba wa mwaka mmoja ambao umemfanya mchezaji huyo kuweza kuchukua kitita cha Dolla za Kimarekani 35,000 sawa na Milioni 58 za Kitanzania.
Kwa upande wa pili, Mchezaji huyo ambaye weekend hii alifunga ndoa ya Kimila huko kwao Uganda na mchumba wake wa zamani, ameahidi kukatisha Fungate na sasa anatarajia kuingia nchini mapema tofauti na ilivyotarajiwa.
Lengo ni kuwahi mchezo wao wa raundi ya nane dhidi ya Kagera Sugar ambao umepangwa kufanyika Desemba 26 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Simba ambayo inakamata nafasi ya saba baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare michezo sita, imekuwa ikisumbuliwa sana na timu ya Kagera Sugar ambayo kwa sasa inakamata nafasi ya tano kwenye ligi kuu na ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa Yanga kwa bao 1-0 kule Kaitaba.
0 comments:
Post a Comment