Chelsea na Arsenal zaangukia pua EPL.
Na Chikoti Cico
Ligi kuu nchini Uingereza iliendelea siku ya Jumamosi kwa mechi mbalimbali huku kwenye uwanja wa St James Park Newcastle United waliialika timu ya Chelsea na mchezo huo kuisha kwa Newcastle kushinda kwa magoli 2-1 na kuvunja rekodi ya Chelsea ya kutokufungwa toka kuanza kwa msimu huu.
Mpaka kipindi cha kwanza kilipoisha matokeo yalikuwa 0-0 huku timu zote mbili zikishindwa kutumia nafasi chache walizozipata ila walikuwa ni Newcastle walioanza kupata goli kwenye dakika ya 57 ya mchezo mfungaji akiwa Papiss Cisse aliyeingia kuchukua nafasi ya Cabella kwenye dakika ya 53.
Huku Chelsea wakitafuta goli la kusawazisha kwa pasi za haraka haraka na mipira mirefu shambulizi la kushtukiza (counter attack) lakini kwenye dakika ya 78 Newcastle ilipata goli la pili huku mfungaji akiwa ni Papiss Cisse tena.
Baada ya goli hilo la pili Newcastle walibaki nyuma kulinda lango lao kwa zaidi ya dakika 10 za mwisho za mchezo huo huku Chelsea wakibaki kutafuta namna ya kusawazisha magoli hayo na kwenye dakika ya 83 Didier Drogba aliyeingia dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Willian aliipatia Chelsea goli la kufutia machozi baada ya kuunganisha mpira wa adhabu ndogo kutoka kwa Fabregas.
Mpaka mwisho wa mchezo Newcastle waliondoka na ushindi wa magoli 2-1 hivyo kufanya mbio za ubingwa kwenye ligi ya Uingereza kuwa wazi zaidi.
Mechi nyingine ya ligi hiyo ilipigwa kwenye uwanja wa Britannia ambapo Stoke City walikuwa wakipepetana na Arsenal mchezo ulioisha kwa Stoke kukusanya alama zote tatu baada ya kuifunga Arsenal kwa magoli 3-2.
Stoke walianza mchezo huo kwa kasi na kwenye dakika ya kwanza tu ya mchezo waliandika bao la kwanza kupitia kwa Peter Crouch baada ya mpira wa krosi uliyopigwa na Steven Nzonzi kuzagaa kwenye lango la Arsenal na kumkuta Crouch huku wakiendelea kushambulia kwa kasi dakika ya 35 Bojan Krkic aliiandikia Stoke goli la pili akiunganisha krosi iliyopigwa na Jonathan Walter.
Dakika zikiyoyoma kuelekea mapumziko walikuwa ni Stoke tena waliopata goli kwenye dakika ya 45 mfungaji akiwa ni Walter akiunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na Crouch baada ya Stoke kupata kona iliyochongwa na Bojan. Hivyo Stoke walienda mapumziko wakiongoza kwa magoli 3-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Arsenal kutaka kurejesha magoli hayo matatu na kwenye dakika ya 46 kocha Wenger alimwingiza Danny Welbeck kuchukua nafasi ya Hector Bellerin ili kuongeza mashambulizi zaidi na dakika ya 63 akamtoa Giroud na kumwingiza Lucas Podolski mabadiliko yaliyoiongezea nguvu timu ya Arsenal.
Na kwenye dakika ya 68 Santi Carzola aliipatia Arsenal goli kwa njia ya penati baada ya Flamini kuonekana kuangushwa kwenye eneo la hatari na Diouf, goli hilo liliamsha ari ya washika bunduki hao wa jiji la London hivyo kuzidi kuongeza mashambulizi kuelekea langoni mwa Stoke City na dakika ya 70 Aaron Ramsey akaipatia Arsenal goli la pili akiunganisha mpira wa kona.
Huku Arsenal wakijitahidi kupata goli la tatu beki wa katikati Chambers akaonyeshwa kadi ya pili ya njano na hivyo kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumshika Bojan wa Stoke wakati akielekea golini, tukio lililosababisha kasi ya Arsenal kupungua.
Hivyo hadi mwisho wa mchezo uwanja wa Britannia ukaendelea kuonekana kuwa mgumu kwa Arsenal kupata ushindi kwa mechi hiyo kuisha kwa magoli 3-2.
0 comments:
Post a Comment