Na Chikoti Cico
Nyasi za uwanja wa Liberty zitawaka moto siku ya Jumapili pale Swansea City watakapoikaribisha Arsenal kwenye mfululizo wa mechi za ligi kuu nchini Uingereza huu ukiwa ni mchezo wa 11 kwa kila timu.
Timu ya Swansea City inayofundishwa na kocha Gary Monk mpaka sasa inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 15 katika michezo 10 waliyocheza huku wakipitwa na Arsenal kwa alama mbili tu hivyo kama wakishinda mchezo huo wataweza kuwa juu ya Arsenal kwa alama moja.
Swansea City watamkosa kiungo Jonjo shelve ambaye anatumikia adhabu baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Everton mchezo ulioisha kwa sare ya bila kufungana hivyo nafasi yake inaweza kuchukuliwa na Tim Carroll.
Takwimu zinaonyesha katika michezo mitano waliyocheza nyumbani timu ya Swansea imeshinda michezo mitatu, kutoka sare mchezo mmoja na kufungwa mchezo mmoja hivyo takwimu hizi zinaonyesha jinsi gani Swansea walivyokuwa bora kwenye uwanja wao wa Liberty.
Wakati huo huo mshambuliaji Wilfried Bony ambaye ana magoli manne mpaka sasa anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya kocha Gary Monk.
Kikosi cha Swansea City kinaweza kuwa hivi: Fabianski; Rangel, Fernandez, Williams, Taylor; Carroll, Ki, Routledge, Sigurdsson, Montero; Bony
Nao washika bunduki wa London timu ya Arsenal wanarejea kwenye michezo ya ligi kuu nchini Uingereza baada ya kucheza katikati ya wiki dhidi ya Anderlecht kwenye moja ya mechi za ligi ya mabingwa Ulaya mchezo ulioisha kwa sare ya magoli 3-3.
Kocha wa Arsenal Mfaransa Arsene Wenger atamkosa kiungo Mikel Arteta ambaye aliumia kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Anderlecht ya Ubelgiji hivyo Jack Wilshere aliyekosekana kwenye mechi mbili za ligi, anatarajiwa kuchukua nafasi ya Arteta kuiongezea makali safu ya kiungo ya Arsenal, naye winga Theo Walcott yuko fiti kuweza kuanza mchezo huo baada ya kuwa nje kwa muda mrefu.
Arsenal ambao wanashika nafasi ya nne wakiwa na alama 17 kwenye msimamo wa ligi rekodi yao ugenini inaonyesha wamecheza michezo mitano na kushinda michezo miwili, kutoka sare michezo miwili na kupoteza mchezo mmoja.
kwa rekodi hizi, kocha Wenger anaonekana kupata matokeo ya wastani ugenini.
Kikosi cha Arsenal kinaweza kuwa hivi: Szczesny, Bellerin, Chambers, Mertesacker, Gibbs; Wilshere, Ramsey, Walcott, Sanchez, Cazorla; Welbeck
0 comments:
Post a Comment