Searching...
Image and video hosting by TinyPic
8 November 2014
Saturday, November 08, 2014

Msuva kuondoka klabu ya Yanga.


Na Oscar Oscar Jr

Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Yanga, Simon Msuva ameripotiwa kuondoka kwenye klabu hiyo. Msuva ni moja kati ya wachezaji tegemeo wa klabu ya Yanga na pamoja na kuwa amekuwa akitumiwa kama mchezaji wa akiba, amekuwa ni mtu anayebadilisha matokeo kila anapopewa nafasi.

Kwa mujibu wa Gazeti la Dimba la leo, mshambuliaji huyo anawindwa na timu za Simba na Azam lakini huenda timu hizo zikagonga mwamba kwani mshambuliaji huyo bado ana mkataba na klabu yake wa miaka miwili.

Mkataba wa Msuva ulimalizika mwishoni mwa msimu uliopita kama ilivyokuwa kwa Didier Kavumbagu na Frank Domayo ambao waliamua kujiunga na timu ya Azam. Hali ilikuwa tofauti kwa Msuva ambaye hakutaka kuondoka na badala yake, akaamua kusaini mkataba mpya wa miaka miwili.

Simon Msuva ameendelea kuonyesha kiwango cha juu hali iliyopelekea timu za Azam na Simba kuanza kummezea mate. 

Kiungo huyo alifanikiwa kubadilisha matokeo kwenye mchezo wa ngao ya Jamii dhidi ya Azam na kuifanya Yanga kuibuka na ushindi wa bao 3-0 akitokea benchi.

Ubora wake hivi karibuni ulionekana pia kwenye mchezo wa Yanga hapo jana walipocheza na timu ya Mgambo ambapo alitoka benchi na kufunga magoli mawili na kufanya mchezo umalizike kwa mabao 2-0.

Yanga kwa sasa, wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara wakiwa na alama 13 nyuma ya Azam nao wakiwa na alama 13 huku, Mtibwa Sugar ambao wanaongoza wakiwa na alama 14 baada ya mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar kuahirishwa hapo jana.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!