Searching...
Image and video hosting by TinyPic
29 November 2014
Saturday, November 29, 2014

Kuelekea mechi ya Southampton vs Manchester City


Na Chikoti Cico

Moja ya mechi zitakazopigwa siku ya Jumapili ni kati ya Southampton dhidi ya Manchester City, mchezo utakaozikutanisha timu mbili zinazokimbizana kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Uingereza huku Southampton ikishika nafasi ya pili na City wakishika nafasi ya tatu kwa tofauti ya alama mbili.

Southampton wanaingia kwenye mchezo huo huku wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja kwenye uwanja wao wa St Mary’s huku wakiwa na alama 26 na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakipitwa kwa alama sita na vinara wa ligi hiyo timu ya Chelsea ambao wanashika nafasi ya kwanza wakiwa na alama 32.

Kocha wa Southampton Mdachi Ronald Koeman ataingia kwenye mchezo huo kutafuta alama tatu muhimu ili kuendelea kujikita kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo.

wakati huo huo, kocha huyo atawakosa James Ward-Prowse, Sam Gallagher na Jay Rodriguez ambao ni majeruhi huku kiungo Steven Davis ambaye anasumbuliwa na misuli akiwa kwenye hatihati ya kutokucheza mchezo huo.

Takwimu zinaonyesha Southampton wameshinda michezo sita na kutoka sare michezo miwili kati ya michezo nane iliyopita waliyocheza nyumbani huku wakifungwa magoli mawili tu katika michezo hiyo, na takwimu hizi ndizo zinaifanya timu hiyo kuingia kwenye mchezo dhidi ya City wakijiamini katika kutafuta alama tatu muhimu.

Kikosi cha Kocha Koeman kinaweza kuwa hivi: Forster; Clyne, Fonte, Alderweireld, Bertrand; Wanyama, Schneiderlin, Tadić; Long, Mane, Pelle

Manchester City kwa upande wao baada ya kupata ushindi muhimu kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo dhidi ya Southampton wakiwa na hamasa ya kutafuta alama tatu muhimu hasa baada ya kuwa na matokeo mabovu katika mechi za karibuni.

Mpaka sasa City wanashika nafasi ya tatu wakiwa na alama 24 kwenye msimamo wa ligi, tofauti ya alama nane na vinara wa ligi hiyo timu ya Chelsea.

City inayofundishwa na kocha Manuel Pellegrini itawakosa mshambuliaji Edin Dzeko, Kiungo David Silva na beki Aleksandar Kolarov ambao ni majeruhi katika mchezo huo dhidi ya Southampton.

Viungo Yaya Toure na Fernandinho ambao walikuwa nje kutumikia adhabu ya kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Bayern Munich, wanatarajiwa kurejea kikosini.

Safu ya ushambuliaji ya Manchester City inatarajiwa kuongozwa na Sergio Aguero ambaye katika mchezo dhidi ya Bayern Munich alifunga magoli matatu (hattrick) hivyo kufikisha jumla ya magoli 14 katika michezo 12 aliyoichezea Manchester City.

Wakati huo huo, mshambuliaji huyo kama atacheza dhidi ya Southampton ataweza kufikisha michezo 100 akiwa na jezi ya Manchester City.

Kikosi cha Kocha Pellegrini kinaweza kuwa hivi: Hart; Sagna, Kompany, Mangala, Clichy; Fernandinho, Navas, Toure, Milner, Jovetic; Aguero

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!