Na Chikoti Cico
Baada ya kutoka sare kwenye mchezo uliopita dhidi ya QPR, timu ya Manchester City itaikaribisha Swansea City kwenye uwanja wake wa nyumbani Etihad katika moja ya mechi za ligi kuu nchini Uingereza zitakazopigwa mwishoni mwa wiki hii.
Wakicheza michezo sita katika mashindano mbalimbali na kushinda mchezo mmoja tu, timu ya Manchester City inatarajia kuingia kwenye mchezo huo dhidi ya Swansea City kutafuta alama tatu muhimu ili kupunguza tofauti ya alama nane dhidi ya vinara Chelsea wenye alama 29.
Manchester City ambao wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 21, watawakosa kiungo David Silva, beki wa kushoto Aleksander Kolarov na mshambuliaji Edin Dzeko ambao ni majeruhi.
Kurejea kwa beki wa katikati na nahodha, Vincent Kompany ambaye alikuwa majeruhi kutakiongezea nguvu kikosi cha Manchester City kwenye mchezo huo.
Kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini anatarajia kumtegemea zaidi mshambulaiji wake Sergio Aguero kuongoza safu ya ushambuliaji katika kutafuta alama tatu muhimu kwenye mchezo huo.
Mpaka sasa Aguero anaongoza kwenye orodha ya wafungaji bora wa ligi ya Uingereza akiwa na magoli 12 katika mechi 11 toka msimu uanze.
Wakati huo huo takwimu zinaonyesha katika michezo sita iliyopita dhidi ya Swansea, Manchester City wameweza kushinda michezo minne, kutoka sare michezo mmoja na kufungwa mchezo mmoja.
Kikosi cha kocha Pellegrini kinaweza kuwa hivi: Hart; Zabaleta, Demichelis, Kompany, Clichy; Milner, Fernando, Toure, Nasri; Jovetic, Aguero.
Baada ya kuifunga timu ya Arsenal kwa magoli 2-1 kwenye mchezo uliopita, timu ya Swansea inatarajia kuingia kwenye mchezo huo wakiwa na ari na hamasa ya kutafuta alama tatu muhimu ambapo kama wakishinda watafikisha alama 21 sawa na Manchester City.
Kocha wa Swansea City Gary Monk anatarajia kumtegemea zaidi mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Wilfried Bony kuongoza mashambulizi dhidi ya Manchester City na takwimu zinaonyesha katika mechi mbili zilizopita dhidi ya timu hiyo, Bony amefunga magoli mawili.
Swansea City ambao wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 18, watamkosa beki Federico Fernandez aliyeko majeruhi huku kiungo Jonjo Shelvey akirejea uwanjani baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo dhidi ya Everton.
Pia viungo Wayne Routledge and Nathan Dyer ambao walikosekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Arsenal, wanatarajiwa kuwa fiti kucheza dhidi ya Manchester City.
Kikosi cha Swansea City kinaweza kuwa hivi: Fabianski; Rangel, Bartley, Williams, Taylor; Shelvey, Ki; Montero, Sigurdsson, Routledge; Bony.
0 comments:
Post a Comment