Searching...
Image and video hosting by TinyPic
25 October 2014
Saturday, October 25, 2014

Uchambuzi: West Ham United vs Manchester City


Na Chikoti Cico

Wagonga nyundo wa London timu ya West Ham United itaikaribisha Manchester City nyumbani Upton Park katika moja ya mechi za ligi kuu ya Uingereza zitakazochezwa wikendi hii.

West Ham United wanaoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu ya Uingereza wakiwa na alama 13 huku wakipishana kwa alama nne tu na Manchester City watarajiwa kuingia kwenye mechi hiyo kutafuta alama tatu muhimu ili kujiweka vizuri kati ya timu nne (top four) za juu kwenye msimamo wa ligi huku mshambuliaji Diafra Sakho akitarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya West Ham mpaka sasa ana magoli matano.

Kocha wa West Ham United Sam Allardyce maarufu kama “Big Sam” atawakosa Guy Demel, James Collins na Joey O’Brien ambao ni majeruhi lakini habari njema kwa kocha huyo ni kurejea kwa kiungo Cheikhou Kouyate na beki James Tomkins ambao walikuwa ni majeruhi.

Mshambuliaji Andy Carroll, pamoja na kurejea mazoezini baada ya kuwa nje akiwa majeruhi kwa muda mrefu bado hajawa fiti kuweza kucheza mchezo huo wa nyumbani dhidi ya City.

Takwimu zinaonyesha katika michezo sita ya ligi iliyopita West Ham United iliyocheza dhidi ya Manchester City imepoteza michezo mitano na kutoka sare mchezo mmoja tu.

Kikosi cha Kocha Big Sam kinaweza kuwa hivi: Adrian; Jenkinson, Reid, Tomkins, Cresswell; Song, Noble, Nolan, Downing; Sakho, Valencia

Baada ya kuwa na matokeo yasiyoridhisha kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya timu ya Manchester City inarejea kwenye mechi dhidi ya West Ham kutafuta alama tatu muhimu na kuendelea kuwakimbiza vinara Chelsea wanaoongoza ligi hiyo.

Mshambuliaji Sergio Aguero anatarajiwa kuendeleza makali yake kwani mpaka sasa ana magoli tisa huku manne kati yao, akiyafunga kwenye mechi za ugenini.

Manchester City ambao wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama 17 kwenye msimamo wa ligi wataendelea kuwakosa viungo Frank Lampard na Samir Nasri ambao ni majeruhi huku wakitarajiwa kuwa fiti kurejea uwanjani kuanzia wiki ijayo.

Wakati huo huo, kocha Manuel Pellegrini anatarajia kuendeleza rekodi ya kutokufungwa ugenini toka kuanza kwa ligi.

Kikosi cha Manchester City kinaweza kuwa hivi: Hart; Zabaleta, Kompany, Mangala, Clichy; Milner, Fernandinho, Toure; Silva, Aguero, Dzeko.

Takwimu zinaonyesha kati ya mechi 90 za ligi kuu ya Uingereza zilizowakutanisha West Ham United na Manchester City, City wameshinda michezo 43 na West Ham wakishinda michezo 33 na wametoka sare michezo 14

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!